WAKATI timu zikiwa zimebakiza michezo saba kila moja kukamilisha mzunguko mmoja wa Ligi ya kikapu Dar es Salaam (BDL), shughuli ni nzito kwa wafungaji kutokana na ushindani mkubwa uliopo.
Nyota wanaowania ufungaji bora hadi sasa ni Ntibonela Bukeng (Savio), Godfrey Swai, (Savio), Yasini Shomari (Mgulani JKT), Enerico Maengela (ABC), Jamel Marbuary (Dar City) na Jonas Mushi (Stein Warriors).
Nyota hao wanaocheza nafasi ya namba tatu ‘Small forward’, sifa zao ni wepesi wa kukimbia na kufunga
Small Forward ni mchezaji anatakiwa kuwa na uwezo wa kukimbia kwa haraka na kufunga (Fast break), kama kwenye soka inavyoitwa ‘Counter attack’.
Kwa upande wa ufungaji, Bukeng wa Savio anaongoza kwa kufunga pointi 213, na anasifika kwa uwezo wa kufunga kwa kutumia mkono wa kulia au wa kushoto.
Swai pia wa Savio anashika nafasi ya pili kwa pointi 159, na ana uwezo wa kufunga katika maeneo ya mtupo mmoja wa three pointi, pamoja na kwenye mazingira ya katikati ya walinzi.
Shomari wa Mgulani JKT, licha ya timu yake kushika nafasi ya mwisho katika msimamo wa ligi, anashika nafasi ya tatu na ana uwezo wa kufunga katika eneo la pointi mbili.
Maengela wa ABC ni wa nne akifunga pointi 136 na ana uwezo wa kufunga katika eneo lote la uwanja.
Marbuary wa Savio, anashika nafasi ya tano kwa pointi 135 na ana uwezo wa kupenya katikaka ya walinzi na kufunga pamoja na maeneo ya pointi tatu.
Mushi wa Stein Warriors anashika nafasi ya sita kwa pointi 128 na ni mwepesi wa kumtoka adui na kufunga, pia ni fundi wa kufunga katika eneo la pointi tatu.