KESI YA MAUAJI YA MUUZA MADINI MTWARA: Kutoka mipango, mauaji mpaka askari kunyongwa- 11

Hamidu Mwanga kutoka Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, alihitimisha kuwa ushahidi wa Jamhuri umethibitisha kuwa, Mussa Hamis alifariki na kifo chake hakikuwa cha kawaida.

Katika sehemu hii, Jaji Mwanga anazungumzia nafasi ya ushahidi wa kimazingira katika kuamua kiini cha pili cha kuthibitisha shitaka la mauaji ya kukusudia kama maofisa hao saba wa Jeshi la Polisi ndio waliohusika na mauaji hayo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Gilbert Sostenes Kalanje aliyekuwa Mrakibu wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara, Charles Onyango (Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara) na Nicholous Kisinza, Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Ofisa wa Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara.

Wengine ni Marco Chigingozi, Mkaguzi Msaidizi, John Msuya (Mkaguzi na Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara), Shirazi Mkupa (Mkaguzi Msaidizi) na Salim Mbalu alikuwa Koplo.

Wote walishtakiwa kwa kosa la kumuua kwa kukusudia, mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis, mkazi wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi Januari 5, 2022, ndani ya Kituo cha Polisi Mitengo  wilayani  Mtwara.

Nani waliohusika na mauaji?

Jaji alisema kabla ya kuamua kama washitakiwa ndio waliohusika na mauaji ya Mussa au la, kwanza anazungumzia nafasi ya ushahidi wa mazingira ambao Jamhuri iliuegemea katika kuthibitisha uhusika wa washtakiwa katika mauaji hayo.

“Kuhusu kiini cha pili, suala linalohitaji majibu ni je, watuhumiwa walioko mbele ya Mahakama hii wanahusika na kifo cha Musa Hamis Hamis?”alisema Jaji.

“Ni wazi kuwa kutokana na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka mahakamani, hakuna shahidi yeyote kati ya 28 waliotoa ushahidi aliyeeleza kuwa aliwaona watuhumiwa wakimuua Mussa Hamis Hamis.

“Hivyo basi, uthibitisho unategemea kabisa ushahidi wa kimazingira.Kwa asili yake, ushahidi wa kimazingira huweza kutoa maelezo zaidi ya moja; hivyo basi, kuna haja ya kuzingatia vipande tofauti vya ushahidi vinavyounga mkono kila kimoja kabla ya kufikia hitimisho lolote,”alisisitiza Jaji Mwanga.

“Ni lazima mazingira yote yakichukuliwa kwa pamoja yaoneshe mnyororo kamili usio na mwanya wowote, kiasi kwamba kwa hali ya kawaida ya kibinadamu, kosa hilo la jinai lilitendwa na watuhumiwa na si mtu mwingine yeyote.”

Jaji Mwanga alisema msimamo huu uliwekwa katika kesi ya Armand Guehi dhidi ya Jamhuri, rufaa ya jinai namba 242 ya mwaka 2010.

“Tena, Mahakama ya Rufaa katika kesi ya Gabriel Simon Mnyele dhidi ya Jamhuri, rufaa ya jinai namba 437 ya 2007, iliweka masharti yanayopaswa kutimizwa katika kesi zinazotegemea ushahidi wa kimazingira kwa kuamua kwamba, ni jambo linalokubalika kuwa ili ushahidi wa kimazingira uwe msingi wa hukumu ya hatia, lazima ushahidi huo uonyeshe bila shaka hatia ya mshtakiwa,”alisema Jaji Mwanga.

Vigezo vitatu ushahidi wa mazingira

“Kutokana na kesi hizo rejea, tumeridhika kuwa pale kesi inapojengwa kwa ushahidi wa kimazingira, ushahidi huo lazima utimize vigezo vitatu,”alisema Jaji.

“Mosi, mazingira ambayo hitimisho la hatia linatarajiwa kutolewa, lazima yawe yamebainishwa kwa nguvu na kwa uhakika.

“Pili, mazingira hayo yawe na mwelekeo mahsusi unaoelekeza moja kwa moja kwenye hatia ya mshtakiwa. Tatu, mazingira yakichukuliwa kwa jumla wake lazima yawe mnyororo kamili usio na mwanya unaoruhusu hitimisho jingine, kwamba kwa hali ya kawaida ya kibinadamu, kosa lilitendwa na mshtakiwa na si mwingine yeyote.

“Hivyo basi, upande wa mashtaka una wajibu wa kuwasilisha ukweli wa kukanusha hali ya kutokuwa na hatia ya mshtakiwa, na ambao hauwezi kuelezwa kwa njia nyingine ya kueleweka isipokuwa kwa hatia ya mshtakiwa,”alisema Jaji.

Jaji alisema kabla ya kutoa hitimisho la hatia kwa msingi wa ushahidi wa mazingira, ni wajibu wa Mahakama kuhakikisha kuwa, hakuna mazingira mengine yanayoshirikiana yanayoweza kudhoofisha au kuondoa hitimisho hilo.

Kwa mujibu wa Jaji Mwanga, katika kesi ya Shilanga Bunzali dhidi ya Jamhuri, rufaa ya jinai namba 30/600 ya mwaka 2020, Mahakama ya Rufani ilijadili kanuni zinazoongoza matumizi ya ushahidi wa mazingira, ambapo ilisema kuwa:

“…Msimamo wa kisheria ni kuwa, mosi; ushahidi wa mazingira unaozingatiwa lazima uwe ni wa hali zinazozunguka tukio, ambazo kwa bahati isiyo ya kawaida, zinaweza kuthibitisha hoja kwa usahihi kama wa hesabu.

“Mbili, kila kiungo katika mlolongo wa ushahidi lazima kichunguzwe kwa makini, na iwapo mwisho wake hautoi hitimisho lisilozuilika la hatia ya mshitakiwa, mlolongo wote wa ushahidi lazima utupiliwe mbali,”alisema Jaji Mwanga akirejea pia shauri la Samson Daniel dhidi ya Jamhuri (1934) EACA 154.

Tatu kwa mujibu wa Jaji ni kwamba, ushahidi lazima uoneshe hatia ya mshitakiwa bila shaka yoyote kwa mtu mwingine yeyote na akarejea shauri la Shaban Mpunzu @ Elisha Mpunzu dhidi ya Jamhuri, rufaa ya jinai namba 12 ya 2002.

“Nne, ukweli unaolenga kutoa hitimisho linalomwathiri mshitakiwa lazima uthibitishwe bila shaka yoyote ya msingi na uhusishwe moja kwa moja na ukweli unaotumika kutoa hitimisho hilo. Angalia Ally Bakari dhidi ya Jamhuri (1992) TLR 10 na Aneth Kapazya dhidi ya Jamhuri, rufaa ya Jinai namba 69 ya 2012.

“Tano, mazingira hayo lazima yawe ya kutoa uhakika wa kimaadili bila shaka yoyote ya msingi. Angalia shauri la Simon Msoke dhidi ya Jamhuri (1958) EA 715.

“Zaidi ya hayo, ni muhimu kutambua kuwa, ushahidi wa mazingira unaweza kuwa na uzito zaidi kuliko ushahidi wa mashahidi wa macho,” alisema Jaji na kurejea kesi ya Georgina Masala dhidi ya Jamhuri, rufaa ya jinai namba 128 ya mwaka 2014.

Jaji alirejea pia kesi ya Samson Daniel dhidi ya Jamhuri (1934) 1 EACA 46, akisema, Mahakama ilieleza kuwa,  “ushahidi wa mazingira unaweza kuwa sio tu wenye uzito sawa bali hata zaidi ya ushahidi wa mashahidi wa macho.”

Jaji alivyopanga washitakiwa kwa makundi

“Nikirejea kwenye kesi hii, ili kuwezesha uamuzi sahihi zaidi wa kiini cha pili cha kama washtakiwa ndio waliohusika na mauaji hayo au la, napendekeza kuwatambua washtakiwa kwa makundi matatu tofauti.

“Mosi, maofisa wa ujasusi na wachunguzi, ambao ni mshitakiwa wa tatu Kisinza, mshtakiwa wa nne,Inspekta Msaidizi Chigingozi, mshtakiwa wa sita Inspekta Msaidizi Mkupa na mshtakiwa wa saba, Koplo Mbalu.

“Mbili, Daktari wa hospitali, ambaye ni mshitakiwa wa tano, inspekta Msuya na tatu ni ni wapelelezi, ambao ni wakuu wa upelelezi kituo Kikuu cha Polisi Mtwara Kalanje na mshtakiwa wa pili, Onyango.

“Uchambuzi wangu utaanza kwa kufafanua majukumu yao katika uchunguzi wa kesi ya jinai dhidi ya mauaji ya Musa Hamis Hamis  kabla ya kubaini iwapo walihusika katika kifo chake au la,”alisema Jaji Mwanga.

Usikose kufuatilia kesho sehemu inayofuata 

Related Posts