Kesi ya mgawanyo wa rasilimali Chadema kunguruma leo

Dar es Salaam. Kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali inayokikabili Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kusikilizwa leo Alhamisi, Julai 10, 2025 Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

Kesi hiyo imefunguliwa na Said Issa Mohamed, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa  chama hicho Taifa, Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, ambao ni wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho kutokea Zanzibar.

Wadaiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa  na Jaji Hamidu Mwanga ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema,  mdaiwa wa kwanza na Katibu Mkuu wa Chadema, mdaiwa wa pili.

Mahakama hiyo inatarajia leo Julai 10, 2025  kutoa hoja kufafanua madai yao ya msingi na wadaiwa nao kujibu hoja za wadai.

Katika kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025, wadai wanadai kumekuwa na  mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara.

Pia wanadai kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia; pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivyo, wanaomba Mahakama hiyo iamuru kwamba wadaiwa wamekiuka Katiba ya chama hicho na kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019 na iwaelekeze kuzingatia sheria hiyo na katiba yake.

Pia, wanaiomba Mahakama hiyo itamke kwamba ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar unaofanywa na wadaiwa  ni kinyume cha sheria na ni batili.

Amri nyingine wanazoziomba ni kusitishwa kwa muda kwa shughuli zote za kisiasa hadi hapo kutakapokuwepo na utekelezaji wa maagizo ya Mahakama, amri ya zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi adaiwa watakapotekeleza matakwa ya sheria husika.

Zuio la muda tayari lilikwisha amri na utekelezaji wake unaendelea ambapo Chadema hakifanya shughuli za kisiasa. 

Vilevile wanaiomba Mahakama iamuru, wadaiwa walipe gharama za kesi hiyo na itoe nafuu nyingine yoyote ambayo  itaona inafaa kuzitoa.

Endelea kufuatilia Mwananchi

Related Posts