KIUNGO mkabaji wa zamani wa KMC, Pascal Mussa ameziingiza vitani Namungo na JKT Tanzania zinazoiwania saini yake baada ya kumalizana na waajiri wake wa zamani.
Mussa tayari amewaaga KMC na amelithibitishia Mwanaspoti tayari ana ofa mbili mkononi kutoka Namungo na JKT Tanzania na mazungumzo baina ya pande zote mbili yanaendelea vizuri.
Akizungumza na Mwanaspoti, alisema alikuwa na furaha KMC na sasa ameamua kutoka ili kujaribu maisha mengine nje ya timu hiyo huku akizitaja JKT Tanzania na Namungo ndiyo zilizoonyesha nia ya kumhitaji.
“Mazungumzo yanaendelea vizuri, nitasaini na moja kati ya timu hizo mbili kama mambo yataenda kama yalivyopangwa, matarajio ni makubwa kutokana na hatua ilipofikia,” alisema kiungo huyo na kuongeza;
“Kucheza timu za madaraja ya chini kwa muda mrefu siyo afya kwa mchezaji, hakukuwa na ubaya wowote. KMC pia walikuwa na nafasi ya kuniongezea mkataba lakini nimeomba kujaribu maisha nje ya timu yao.”
Pascal alisema anahitaji kucheza timu ambayo itampa changamoto ya namba ili aendelee kukuza kipaji chake na anaamini kila timu kuna wachezaji wazuri na hilo halitamnyima nafasi ya kucheza kama ataonyesha nini anakihitaji kwa wakati sahihi.
“Kwenye kila kazi kuna changamoto, sihofii mchezaji yeyote kwa sababu napenda ushindani na ili kuwa bora lazima ukutane na mshindani. Nipo tayuari kupambania nafasi.”