Maboresha ya bandari yachochea biashara ya kemikali ndani, nje

Dar es Salaam. Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), imesema maboresho ya miundombinu ya bandari za Dar es Salaam na Tanga yamechangia ongezeko la biashara ya kemikali nchini, hasa zile za kimkakati zinazotumika katika uchimbaji na uchenjuaji madini ndani na nje ya nchi.

Sababu nyingine ya ongezeko hilo imetajwa kuwa ni mahusiano mazuri kati ya Tanzania na mataifa ya jirani yaliyowekwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumzia mafanikio ya mamlaka hiyo katika mkutano na wanahabari ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko amesema mamlaka hiyo imeendelea kuchangia uboreshaji wa mazingira ya biashara ya kemikali hizo zinazotumika nchini na mataifa jirani ya Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Dk Mafumiko katika mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam amesema kemikali ya Ammonium Nitrate inayotumika katika ulipuaji wa miamba wakati wa uchimbaji madini nchini, Zambia na DRC imeongezeka kutoka tani 135,445 mwaka 2021/22 hadi tani 461,777.42 kufikia Juni, 2025 sawa na ongezeko la asilimia 241.

“Mamlaka imewezesha zaidi ya asilimia 80 ya shehena ya Ammonium Nitrate iliyoingizwa nchini kupitia Bandari ya Tanga, hivyo kuongeza thamani ya uwekezaji uliofanywa na Serikali kwa kuongeza kina cha bandari hiyo,” amesema.

Dk Mafumiko amesema kemikali ya salfa inayotumika katika mchakato wa uchimbaji na uchenjuaji wa madini ya shaba Zambia na DRC, uingizwaji kupitia Bandari ya Dar es Salaam umeongezeka kutoka tani 396,982 mwaka 2021/22 hadi tani 1.867 milioni kufikia Juni, 2025 sawa na ongezeko la asilimia 370.32.

Amesema kemikali ya Sodium Cyanide inayotumika katika uchenjuaji wa madini ya dhahabu nchini, Zambia na DRC ambayo uingizwaji wake hupitia Bandari ya Dar es Salaam imeongezeka kutoka tani 41,461 mwaka 2021/22 na tani 63,103.4 kufikia Juni, 2025 sawa na ongezeko la asilimia 52.20

Amesema kupitia mpango wa elimu kwa umma unaotekelezwa na mamlaka kwa wadau wa biashara ya kemikali kumekuwa na ongezeko kubwa la wadau wanaotimiza matakwa ya sheria ya usimamizi na udhibiti wa kemikali.

Vilevile amesema kumekuwa na ukuaji wa biashara kwa wadau wanaojihusisha na biashara ya kemikali, ambao waliosajiliwa wameongezeka kutoka 2,125 mwaka 2021 hadi 3,835 kufikia Juni, 2025 sawa na ongezeko la asilimia 81.

Kuhusu ukaguzi wa maghala katika kuhakikisha kemikali zinatumika kwa usalama na kwa kufuata taratibu zinazohitajika amesema mamlaka imekagua maghala 8,521 ya kuhifadhia kemikali sawa na asilimia 119 ya lengo la kukagua maghala 7,160.

Ukaguzi hufanyika ili kulinda afya ya binadamu na mazingira, pia kuhakikisha kemikali zinazoingizwa nchini ni zile ambazo zinaruhusiwa kisheria kuingia.

Mbali na hayo, Dk Mafumiko  amesema kumekuwa na ongezeko la vibali vya uingizaji kemikali kutoka 40,270 mwaka 2020/21 hadi 67,200 kufikia mwaka 2024/25 sawa na ongezeko la asilimia 40 ya vibali vilivyotolewa.

“Ongezeko hili la vibali limetokana na kuwepo mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji yaliyowekwa na Serikali, wadau kuongeza uelewa wa sheria, kanuni na miongozo inayosimamia shughuli za kemikali kwa kujengea uelewa wa matumizi sahihi ya mifumo ya Tehama inayotumika katika uombaji wa usajili na vibali,” amesema.

Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa mamlaka hiyo, Daniel Ndiyo amesema kuongezeka kwa uingizaji wa kemikali za viwandani kumezalisha ajira zaidi na kuongeza mapato ya kodi.

“Tani zaidi maana yake ni ajira zaidi kwa madereva wa malori, shughuli nyingi zaidi bandarini na upatikanaji rahisi wa kemikali muhimu za uchimbaji madini. Mambo haya kwa pamoja yanachochea ukuaji wa uchumi,” amesema.

Katika hatua nyingine, Dk Mafumiko amesema kumekuwa na ufanisi katika utoaji huduma za uchunguzi wa kimaabara katika miaka minne ya Serikali chini ya Rais Samia akieleza uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara kwa sampuli/vielelezo umeongezeka kutoka sampuli 155,817 mwaka 2021/22 hadi 188,362 mwaka 2023/24, sawa na ongezeko la asilimia 21.

Amesema katika mwaka 2024/25, kuanzia Julai hadi Mei 2025, sampuli 175,561 zilifanyiwa uchunguzi sawa na asilimia 92 ya lengo la kuchunguza sampuli 191,420.

Amefafanua kuwa ongezeko hilo linatokana na kuongezeka uelewa wa wananchi na wadau wa mamlaka na ubora wa huduma za uchunguzi zitolewazo.

Vilevile, amesema linatokana na ushirikiano na taasisi za Serikali za udhibiti kama vile Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wadau wa afya zikiwemo hospitali, Usalama Mahali pa Kazi (Osha), Baraza la Taifa la Hifadhi na

Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na wadau wengine wanaotumia huduma za mamlaka hiyo ili kupata uhakika wa ubora wa bidhaa zao.

Related Posts