MABOSI wa Polisi Tanzania wamempa mkataba wa miaka miwili, Mbwana Makatta, baada ya kocha huyo kutokuwa na timu tangu mara ya mwisho alipoachana na Tanzania Prisons Desemba 28, 2024, kutokana na mwenendo mbaya katika Ligi Kuu Bara.
Makatta aliyewahi kuinoa Polisi Tanzania, alitambulishwa Julai 9, 2025, Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Kamishna wa Polisi Jamii, CP Faustine Shilogile, huku lengo kubwa ni kuhakikisha timu hiyo inarejea tena Ligi Kuu Bara.
Akizungumza na Mwanaspoti, Makatta alisema ni fahari kubwa kuaminiwa na kupewa nafasi hiyo, ingawa haitokuwa kazi nyepesi ya kufanikisha malengo hayo, ikiwa hakutokuwa na mshikamano wa pamoja wa kutengeneza kikosi cha ushindani.
“Naamini tunaweza kufikia malengo na jambo nzuri nimeshawahi kufanya kazi hivyo natambua kiu ya uongozi ni nini, ni wazi haitokuwa rahisi ila kwa ushirikiano ambao nimeahidiwa, sina shaka msimu wa 2025-2026 tutafanya vizuri,” alisema Makatta, kipa wa zamani wa Tukuyu Stars na Yanga.
Kabla ya kutua Polisi, Makatta aliiongoza Prisons katika mechi 14 za Ligi Kuu Bara na alishinda mbili tu, sare mitano na kupoteza saba, kisha kuondoka na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa Kocha wa Geita Gold, Amani Josiah.