Dar es Salaam. Katikati ya dhana kuwa kuimarika kwa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) kutawaathiri wamiliki wa daladala, Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), umesema tayari utaratibu maalumu umepangwa kuhakikisha biashara ya wasafirishaji hao haiathiriki.
Mtendaji Mkuu wa Udart, Dk Athumani Kihamia amesema utekelezwaji wa utaratibu huo, utahusisha kuundwa kwa kampuni ili daladala zote ziwe katika mfumo rasmi, badala ya ilivyo sasa kila daladala ikinunuliwa inatafuta njia yake.
Hata hivyo, wakati mradi wa awamu wa kwanza ulipokaribia kuanza kazi, kwa mujibu wa wamiliki wa daladala mkoani utaratibu uliotumika kuwaondoa ulihusisha mwekezaji aliyelipa fidia ya Sh4 milioni kwa kila daladala iliyokuwa inafanya kazi katika njia hiyo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti Chama cha Wasafirishaji Mkoa wa Dar es Salaam (Uwadar) kipindi hicho, Gharib Mohamed amesema katika fedha hizo walikubaliana Sh3 milioni walipwe moja kwa moja na Sh1milioni iliyobaki ziingizwe kwenye umiliki wa hisa wa Kampuni ya Udart wakati huo, ikiwa chini ya mwekezaji Robert Kisena.
Jingine walilokubaliana Mohamed amesema ni kuundwa kwa kampuni zinazotokana na wamiliki wa daladala zilizotoa Kampuni ya Uwadar na Kampuni ya Wazawa, lengo likiwa kuwa miongoni mwa wawekezaji watakaoleta mabasi yao katika mradi huo, lakini mwisho wa siku hilo halikufanikiwa.
“Kipindi kile kulikuwa na ushirikishwaji wa hali ya juu kati yetu wamiliki wa daladala, Dart na mwekezaji, tofauti na sasa mambo mengi tunayasikia tu huko mitandaoni au kusoma kwenye magazeti kama watu wengine lakini sio wadau muhimu katika usafirishaji,” amesema Mohamed.
Akizungumzia hilo katika mahojiano maalumu na Mwananchi Jumanne ya Julai 8, 2025, Dk Kihamia amesema:“Wakishaunda kampuni ndio sasa wanamiliki hizo daladala watakazokuwa na hisa kulingana na wingi wa daladala alizonazo mtu na baada ya hapo,Serikali inatarajia kufanya uwezeshaji ikiwamo mafunzo na kuwapatia mikopo ya kununua magari mengi zaidi.”
Wakati kwa upande wa madereva, amesema hilo watafaidika nalo kwa kuwa wataanza kulipwa mishahara tofauti na sasa hivi, mtu akichukua daladala jioni anapeleka hesabu kwa tajiri.
“Dereva huyu hatujui siku ambayo hajapata au kapigwa faini na kosa labda ni gari, anafukuzwa kazi na wakati huo ana familia inamtegemea kupitia kazi hiyo,” amesema Dk Kihamia.
Katika kulitekeleza hilo, amesema wanashirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) na Wizara ya Uchukuzi na Ofisi ya Rais Tamisemi, ingawa vinara wakubwa hapa ni Dart, ili kuhakikisha hilo jambo linafanikiwa.
“Hili lipo kwenye mipango yetu ya kibajeti na kimipango, kwa hiyo kabla ya mwisho wa mwezi huu tutakutana na wamiliki wa daladala na madereva ili tuweze kujadiliana namna bora ya kuweza kutekeleza hilo.
“Maana kwa kuwashirikisha tu wamiliki peke yao wanaweza wakaelewa wachache na wengine wakabaki kushangaa, kwa sababu pia tumegundua wamiliki wa daladala ni watu wengine kabisa, na watumishi ni wengine, kwa hiyo waathirika wakubwa sio wamiliki bali ni madereva na makondakta wao,” amesema.
Hata hivyo, amekiri kila mabadiliko mwanzoni huwa yakitiliwa shaka lakini haya ana uhakika asilimia mia madereva watakuja kunufaika wao na kuahidi kwamba, mwanzoni wasaidia mpaka pale watakapoona wameweza kusimama wenyewe kwani watawasaidia hadi kifedha ili kuunda kampuni hizo.
Amesema kwa kuwa katika mradi huo wa mwendokasi mabasi yao hayatahusika kabisa, lakini kupitia mradi wa ujenzi wa barabara za DMDP zilizotengewa zaidi ya Sh1 trilioni, ana uhakika watapata maeneo ya kuepeleka gari zao na mpaka zitabaki.
Alipoulizwa kuhusu kampuni zilizoundwa katika awamu ya kwanza kama zinaweza kutumika, Dk Kihamia amesema kama itawapendeza kuendelea nazo, itakuwa sawa kwao kama wataona wafungue nyingine nayo heri.
Kwa kufanya hivyo pia amesema wataweza kukopesheka na tayari benki mbalimbali zimeonesha nia ya kukubali hilo na siku moja huenda nao, wakamiliki mabasi yao ya mwendokasi yanayoweza kutumika kuchukua abiria kutoka pembezoni na kuwapeleka barabara kuu.
“Vilevile tayari wafadhili mbalimbali wanaofadhili Serikali katika miradi mbalimbali ya usafiri wameshakubali kufadhili hilo na sasa mshauri mtaalamu wetu yupo kazini kutengeneza baadhi ya vipengele, kimojawapo ni namna bora a daladala zitaendeshwa na akimaliza atatupatia ripoti yake,” amesema.
Walichosema wamiliki, madereva
Wakitoa maoni yao kuhusu hatua hiyo, baadhi ya wamiliki wa daladala na madereva wamesema, ni jambo zuri kwa kuwa ndio ilikuwa ndoto zao za siku nyingi.
“Tulishatoa kilio chetu hiki kuwa nasi tunataka kuwa moja ya wawekezaji katika mradi huo, lakini ikawa kama kilio cha samaki maji kwenda na maji, hivyo kama Serikali imeona hili lina tija kwa sasa tunashukuru,”amesema Break Salim mmoja wa wamiliki wa daladala.
Salim amesema wapo tayari kuwa wawekezaji katika mradi huo huku akiomba wapewe njia moja hata ya majaribio ili Serikali ione kama watashindwa.
Aliyewahi kuwa Mwenyekiti na Mwanzishi wa Uwadar, Ghalib Mohammed amesema kwa kuwa wamebaini madhaifu hayo na kutaka kuyarekebisha wanawasubiri siku wakiitwa watatoa maoni yetu.
Mwenyekiti wa Wamiliki wa Madereva Dar es Salaam (Darcoboa), Sabri Mabrouk amesema katika utekelezaji wa mradi huo, kikubwa wamiliki wanatakiwa kubadilika kuendana na wakati kwa kuwa, katika safari hiyo ya usafirishaji wamepita katika hatua mbalimbali.
“Katika kazi hii ya kutoa huduma za usafiri tumepita katika hatua mbalimbali kuanzia gari aina ya cha maharagwe, baadaye Hiece maarufu vipanya , ikaja DCM, Tata na Hier na sasa mwendokasi, hivyo hatuwezi kushindwa kikubwa ni kukubali kubadilika kuendana na wakati,” amesema Mabrouk.
Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva na Makondakta Mkoa wa Dar es Salaam (Uwamada), Shukuru Mlawa amesema wao wapo mguu sawa kuanza kwa huduma hizo.
Mlawa amesema katika kupata ajira kwenye mradi huo au kampuni zitakazoundwa kama wanavyosema Dart, kila dereva anahitaji, kwa kuwa kazi ya daladala ni ngumu na wanatumia nguvu kubwa katika kufanikisha hesabu za matajari wao.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania(Tadwu), Ally Kimaro amesema suala la mikataba kwa madereva sio jambo geni, kwa kuwa lilishaundiwa na ilipopotelea hawajui.
Kimaro amesema mpaka hapa walipo migogoro ni mingi na hawajui Dart watakuja na sera gani, kwa kuwa hata wizara yenye dhamana na kazi imeshindwa kutatua changamoto hiyo.
“Ushauri wangu kwa sasa katika suala la madereva, zitakapoundwa kampuni wanazozisema ili kuwapa afueni madereva kuwa na mikataba, lakini pia kwa hizo za mwendokasi zitakapoanza kufanya kazi wizara ya kazi ikae mbele kuhakikisha hilo linatekelezeka kivitendo.
“La sivyo, danadana zitakuwa ni zilezile na ukizingatia madereva walivyo mtu ukiacha kazi leo, mwenzako kesho anaenda kufanya kazi hiyohiyo kwa ujira mdogo,”amesema mwenyekiti huyo.
Hata hivyo, amesema wakati kima cha chini cha mshahara kilichopangwa na Serikali kikiwa ni Sh300,000 pamoja na marupurupu mengine ikiwamo huduma za afya, nauli lakini ukweli ni kwamba, kuna wamiliki hata Sh200,000 ya mdomo kulipana na madreva wao kwa mwezi ni kazi.