Polisi Tanzania yapata tumaini kwa Makatta, yaapa kupanda Ligi Kuu

Timu ya Polisi Tanzania imeonyesha dhamira ya dhati ya kufanya vizuri msimu ujao wa Ligi Daraja la Kwanza (Championship), baada ya kumsaini rasmi kocha mwenye uzoefu Mbwana Makatta kwa mkataba wa miaka miwili.

Akizungumza leo Julai 10, 2025 jijini Dodoma, Ofisa Habari wa Polisi Tanzania, Inspekta Frank Lukwaro, amesema uongozi wa timu hiyo umejiridhisha na uwezo wa Makatta, hasa kutokana na historia ya kuipandisha timu hiyo Ligi Kuu msimu wa 2018/2019.

“Makata sio mgeni kwetu, aliwahi kuwa nasi wakati tulipopanda Ligi Kuu msimu wa 2018/2019. Uzoefu wake katika Ligi ya Championship ni mkubwa na anatufahamu vyema, hivyo tunaamini atakuwa na wakati mzuri wa kuturudisha tulikostahili,” amesema Lukwaro

Ameongeza kuwa, tayari Makatta amekabidhiwa ripoti ya msimu uliopita ili iwe chachu ya kujenga kikosi imara kitakachopambana vikali msimu ujao, huku akisisitiza benchi la ufundi litapewa ushirikiano wa kutosha kufanikisha malengo.

“Malengo yetu ni kupanda Ligi Kuu. Tumejipanga kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro, wadau wa michezo pamoja na mashabiki kote nchini, kwa kuwa Polisi Tanzania ni timu ya wananchi wote. Tunataka kuwa na kikosi bora, kisichoishia kuhimili ushindani bali pia kiwe kiwanda cha vipaji,” ameeleza Lukwaro.

Makatta, aliyewahi kuzinoa pia timu mbalimbali ndani ya nchi, alitambulishwa rasmi na Mwenyekiti wa Polisi Tanzania, Kamishna wa Polisi Jamii CP Faustine Shilogile, ambapo alisaini mkataba wa miaka miwili, ishara ya kuaminiwa kwake katika kutimiza ndoto ya kurejea Ligi Kuu Bara.

Kwa hatua hii, Polisi Tanzania inaonekana kuja kwa kasi msimu huu, huku macho yote yakielekezwa kwa Makatta kuona kama ataweza kurudia historia ya mafanikio aliyowahi kuandika na kikosi hicho miaka michache iliyopita.

Related Posts