PPRA kufikia watu milioni tano kutoka makundi maalumu

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) imeweka lengo la kuwafikia Watanzania milioni tano kutoka makundi maalumu yakiwemo wanawake, vijana, wazee, na watu wenye ulemavu kwa kuboresha ushiriki wao katika mchakato wa manunuzi ya umma.

Hayo amesemwa na  Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Denis Simba wakati akizungumza na Mwananchi katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), maarufu kama Sabasaba.

Simba amesema Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2023 na Kanuni zake za mwaka 2024 zimeweka msingi imara wa kuendeleza ujumuishaji wa kiuchumi kupitia matumizi ya fedha za umma.

“Mageuzi yaliyofanyika si zawadi au msaada, bali ni jitihada mahsusi za kurekebisha ukosefu wa usawa wa muda mrefu katika upatikanaji wa fursa za kiuchumi,” amesema.

Amesema sheria hiyo inaelekeza kuwa angalau asilimia 30 ya fursa za manunuzi katika taasisi zote za umma kuanzia Serikali Kuu hadi serikali za mitaa na mashirika ya umma zigawanywe kwa ajili ya makundi maalumu.

Makundi hayo ni ya vijana na watu wenye ulemavu ambao wametengewa asilimia 10 kila kundi huku wanawake na wazee wakipata asilimia tano kila mmoja.

Simba amesema hilo linafanyika kwa sababu Serikali inatambua nafasi ya manunuzi ya umma kama nyenzo ya kuwawezesha wananchi walioko pembezoni.

Katika kufanikisha hilo, PPRA imeanzisha mkakati wa mawasiliano kwa njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari vya kawaida, semina za mtandaoni na ushirikiano na wasanii ili kuongeza uelewa na kuhamasisha ushiriki mkubwa kutoka kwa makundi lengwa.

Takwimu zilizotolewa na mamlaka hiyo zinaonyesha kuwa thamani ya zabuni zilizotolewa kwa makundi haya iliongezeka mara mbili kutoka Sh8 bilioni katika mwaka wa fedha 2023/24 hadi Sh16 bilioni mwaka 2024/25.

Amesema lengo la muda mrefu ni kufikia thamani ya mikataba ya Sh200 bilioni kadri idadi ya walengwa inavyoongezeka.

Hadi sasa, jumla ya makundi maalumu 280 yamesajili na kuwasilisha taarifa zao katika Mfumo wa Kitaifa wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Kielektroniki (NeST) na kupata zaidi ya mikataba 440.

Kati ya mikataba hiyo, makundi yanayoongozwa na vijana yamepata asilimia 58, wanawake asilimia 34, wazee asilimia 6, na watu wenye ulemavu asilimia 2 pekee.

“Tofauti hii ya ushiriki, hususan kwa upande wa watu wenye ulemavu inaonyesha haja ya haraka ya elimu na msaada wa kulenga kundi hilo. Tumepiga hatua, lakini bado tunahitaji kufanya zaidi kuhakikisha kila mmoja anapata fursa sawa,” amesema Simba.

Akizungumza na Mwananchi mmoja wa watembeleaji wa maonyesho hayo, Said Mapunda ameshauri elimu zaidi kutolewa kwa makundi lengwa ili waweze kuzifikia fursa.

“Ukiniambia mimi kuhusu manunuzi ya umma sielewi na kidogo nina angalau nina elimu hadi ya chuo, vipi yule ambaye ni mlengwa na hakupata elimu, nadhani lugha nyepesi zaidi inahitajika kutumika ili watu waelewe,” amesema Mapunda.

Related Posts