MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amempongeza beki wa Yanga, Israel Mwenda kwa mafanikio aliyoyapata msimu huu akiwa na kikosi hicho, huku akimuomba asiondoke klabuni hapo kwa ndio timu bora kwa sasa nchini.
Mwenda amejiunga na Yanga dirisha dogo Januari mwaka huu akitokea Singida Black Stars, ametwaa ubingwa wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho(FA) na Kombe la Muungano.
Mtanda anayefahamika kuwa shabiki wa Yanga, ametoa pongezi hizo leo Jumatano Julai 9, 2025 kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza wakati akizindua bonanza la Alliance Day kusherehekea miaka 25 ya kituo na Shule za Alliance na kuenzi maisha ya mwasisi wa Kituo hicho, James Bwire aliyefariki Januari 26, mwaka huu.
Mwenda pamoja na wachezaji wengine waliolelewa na kupita katika kituo cha Alliance kilichopo Mahina jijini Mwanza wamecheza mchezo wa hisani dhidi ya wachezaji wa Ligi Kuu kutoka timu za Simba, Yanga, Azam na JKT Tanzania ukimalizika kwa sare ya mabao 2-2 kabla ya penalti 4-2 kuipa ushindi kikosi cha mastaa wa Ligi Kuu.
Mtanda amesema mkoa huo unajivunia kuwa na mchezaji kama Mwenda ambao kwa sasa anaitambulisha Mwanza, ambapo amemsihi baba wa mchezaji huyo, Patrick Osoro kuhakikisha mchezaji huyo anatulia Yanga.
”Nakupongeza Mwenda na nimeambiwa baba yake pia yuko hapa, Mzee Mwenda wewe hakikisha Israh bado anaendelea kucheza Yanga, ndio timu bora kwa sasa, hivyo na ukileta maneno maneno hapa tunakuondoa hapa Mwanza uende huko kijijini,” amesema Mtanda na kuongeza; “Tunakupongeza kwanza kwa kubeba Kombe la Ligi Kuu na makombe yote , kwa hiyo amechezea timu bora ambayo tunakupongeza lakini tunawapongeza wachezaji wote ambao wanacheza katika klabu mbalimbali kwa sababu tumewaona viwango vyao vizuri.”
Mtanda ambaye ni mlezi wa timu ya Pamba Jiji, amempongeza mchezaji huyo kwa kulibeba tamasha hilo.
Kwa upande wa Mwenda amesema ameweza kuwashawishi wachezaji wengi wakiwemo wa Yanga kwa sababu ni marafiki zake, huku akiwashukuru wadau na mashabiki wa soka jijini Mwanza kwa kujitokeza kwa wingi katika tamasha hilo.
”Wachezaji waliokuja leo ni washkaji zangu hivyo nilivyowafikishia hili jambo hawakuweza kujiuliza mara mbili lakini pia naushukuru uongozi wa Alliance kwa sababu walianzisha hili wazo na kuandaa kila kitu nami nikajitolea upande wangu kuwashawishi wachezaji kuja,” amesema Mwenda na kuongeza; “Mwisho wa siku sisi tunafanya hili jambo kurudisha kwa jamii sisi tuko ndani ya jamii kwahiyo nadhani ni kitu cha muhimu sana tulichokifanya leo na niwashukuru wana Mwanza kwa kujitokeza.”