Sagini aitaka OCPD kuelimisha jamii mchakato wa utungwaji wa sheria za nchi.

 

 Na:
Calvin Gwabara – Dar es salaam.

Watanzania wametakiwa kutambua
kuwa miswada ya sheria haitoki serikalini pekee bali hata wananchi wanaweza
anzisha mchakato na kupendekeza mswada wa sheria wanayoitaka kutungwa kupitia
wawakilishi wao bungeni.

Mwandishi wa Sheria kutoka OCPD Bwana Vincent Masalu (Wa kwanza kulia) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Jumanne Abdalah Sagini

Kauli hiyo imetolewa na Naibu
Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Jumanne Abdalah Sagini wakati
alipotembelea banda la Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) kwenye Maonesho
ya Kimataifa ya Biashara SABASABA yanayoendelea jijini Dar es salaam ambayo Ofisi
hiyo inashiriki kwa lengo la kutoa elimu ya masuala mbalimbali ya uandishi wa
sheria, ufasili wa sheria pamoja na urekebu.

“Kumekuwa na dhana kuwa miswada
yote ya sheria inaanzishwa na Serikali na hivyo kuwafanya wananchi kuona kama
wanatungiwa sheria tu na serikali bungeni kitu ambacho sio sahihi kwani
wananchi popote walipo nchini wanaweza kuanzisha mchakato wa kutengeneza mswada
wa sheria na kisha kuuwasilisha bungeni kupitia wabunge wao” Alifafanua Mhe.Sagini.

Aliongeza “Niwaombe nyinyi kama
wataalamu kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria kutumia nafasi ya uwepo wenu
kwenye maonesho haya makubwa kuwapatia wananchi elimu ya kina kuhusu mchakato
wa uandaaji wa miswada maana maonesho haya yanawaleta watu wa makundi
mbalimbali ambao wakipata elimu hiyo wataifikisha kwenye jamii zao na hivyo
kuongeza uelewa kwa jamii yetu”.

Aidha Naibu huyo wa Wizara ya
Katiba na Sheria ameipongeza Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria kwa kukamilisha
kufanya urekebu na kutoa toleo la mwaka 2023 lililozinduliwa na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mwezi wanne mwaka huu na
ambalo limeanza kutumika tarehe 1 mwezi wa 7 mwaka huu.

Katika hatua nyingine Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza 
Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga ambaye
ametembelea banda hilo la OCPD kwenye maonesho hayo ameipongeza Ofisi hiyo kwa
kazi kubwa waliyoifanya ya kufanya urekebu wa sheria kuu zote nchini.

Hata hivyo Jaji huyo ametaka
kujua kuhusu kanuni za sheria hizo zilizofanyiwa urekebu kama pia zipo tayari
kwaajili ya matumizi na baada ya kupata majibu ameiomba Ofisi hiyo pamoja na
majukumu mengi waliyonayo ameshauri kuzikamilisha mapema ili nazo ziweze
kupatakana kwa wakati ameishauri ofisi hiyo kuhakikisha zinakamilika.

Kwa upande wake Mwandishi wa
Sheria kutoka OCPD Bwana Vincent Masalu akitoa maelezo na ufafanuzi kwa
viongozi hao amesema tayari Ofisi inaendelea na zoezi la kufanyia kazi kanuni
za sheria hizo ili kuhakikisha zinakwenda sambamba na sheria kuu.

Masalu amesema wataalamu wa Ofisi
hiyo wanafanya kazi usiku na mchana kushughulikia mambo yote bila kuchoka
ikiwemo zoezi la ufasili wa sheria kuu zote ambazo zinatarajiwa kutolewa mwezi
wa nane na hivyo kusadia jamii kupata sheria na kanuni zake.

“Tunatumia fursa ya kuwepo
kwenye  maonesho haya ya sabasaba
kuwafikia wadau wengi zaidi kwakuwa kwenye maonesho haya kuna wadau wote wa
sheria kuanzia Wananchi wa kawaida, Taasisi za kiserikali na Wizara na hivyo
kuwa sehemu muhimu ya kuwafikia wadau wetu na kuwapa elimu ya masuala ya
kisheria kwa maana ya mchakato wa utungwaji hadi kusainiwa na Mhe. Rais kuwa
sheria pamoja kuwaelewesha majukumu yanayotekelezwa na Ofisi yetu ya Mwandishi
Mkuu wa Sheria” alifafanua Masalu.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga akisisitiza jambo kwa Waandishi wa sheria katika banda ya Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria.

Mwandishi wa Sheria kutoka OCPD Bwana Vincent Masalu akifafanua jambo kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga.

Mwandishi wa Sheria kutoka OCPD Bwana Vincent Masalu akimkabidhi zawadi Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga.

Mwandishi wa Sheria kutoka OCPD Bwana Vincent Masalu akimkabidhi zawadi kwa Naibu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Jumanne Abdalah Sagini.

Related Posts