WAKUBWA wa Kariakoo wameanza kuonyeshana ubabe wa matumizi ya fedha, ambapo mabosi wa klabu za Simba na Yanga hivi sasa wanazimwaga ili kunasa mastaa wa maana kwa ajili ya mashindano msimu ujao wa soka.
Nyuma ya ubabe huo unaambiwa kwamba yule kiungo mahiri aliyemaliza mkataba Yanga, Mudathir Yahya amenasa katika mtego wa pande hizo mbili, lakini kinachofanyika mbele yake ni namna wababe hao wanavyoonyesha umwamba wa kuongeza sifuri mbele.
Tayari mabosi wa Simba wameamua, baada ya sasa kumgeukia Mudathir kwa kuongeza dau zaidi ya lile alilowekewa na uongozi wa Jangwani unaozungumza naye ili kumbakisha kikosini.
Yanga ambayo inajiandaa kumtangaza kocha mpya anayechukua nafasi ya Miloud Hamdi aliyetimkia Ismailia ya Misri, inaelezwa ilianza mazungumzo na kiungo huyo wa zamani wa Azam na Singida United, lakini mabosi wa Simba wameamua kuingilia dili hilo kwa kumuweka dau kubwa zaidi mezani.
Mudathir aliyeitumikia Yanga kwa misimu mitatu akiifungua mabao 13 ya Ligi Kuu, inadaiwa bado hajafanya uamuzi wapi atue, lakini dau alilowekewa na mabosi wa Msimbazi limemchanganya kwani limezidi lile wanalojadiliana na timu yake ya sasa.
Mwanaspoti liliwahi kuandika kuwa ripoti ya aliyekuwa kocha wa klabu hiyo Hamdi Miloud ilitaka viungo watatu waongezewe mikataba ambao ni Khalid Aucho, Duke Abuya na Mudathir.
Baada ya hekaheka za ligi na paredi la ubingwa, ndipo mabosi hao walipoamua kukaa naye mezani ili kupiga hesabu za kumpa mkataba aweze kusalia katika timu.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti; “Yanga inataka kumpa Sh100 milioni kama pesa ya kusaini mkataba mpya kisha mshahara wa Sh10 milioni kwa mwezi ofa ambayo Mudathir ameigomea, huku ikielezwa sababu kubwa ni ofa aliyodokezwa na Wekundu wa Msimbazi inayosaka kiungo fundi.”
Inadaiwa kuwa, baada ya Simba kupata uhakika kuwa kiungo huyo amemaliza mkataba na Yanga na kujua dau alilowekewa mezani, ikapiga hesabu kali za kumnasa huku ikiweka mzigo mkubwa mezani zaidi ya Yanga.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kuwa Simba imemtengea dau la Sh150 milioni kwa ajili ya kusaini na mshahara wa Sh15 milioni kwa mwezi, huku ikimwambia akiwa tayari akasaini na kuchukua pesa zake.
Ikumbukwe miaka mitatu nyuma baada ya Mudathir kumalizana na Azam, mabosi wa Simba pia walikuwa wakimmezea mate lakini walichelewa baada ya Yanga kumuwahi.
Hii sio mara ya kwanza kwa Simba kuingilia usajili wa mastaa ambao Yanga inafanya nao mazungumzo kwani hivi karibuni Mwanaspoti liliripoti dili la mshambuliaji Celestin Ecua kutoka ASEC Mimosas imeliingilia. Yanga imemaliza msimu ikiwa kileleni ikifungwa mabao 10 ikifunga 73 ikiongoza kwa kufikisha pointi 82 katika mechi 30 ilizocheza.
Wakati Mudathir akiendelea kusikiliziwa na Wanasimbazi, inadaiwa kuwa mabosi wa Simba wameshamalizana na winga anayemudu kucheza pia kama mshambuliaji wa kati, Mofosse Tresor Karidioula aliyekuwa akikipiga Haras El Hadood ya Misri.
Nyota huyo kabla ya kucheza Misri aliwahi kukipiga Ases Mimosas ya Ivory Coast iliyowauzia Wamisri mwaka 2024, lakini pia amekipiga Wydad Casablanca ya Morocco 2018 na kwa msimu uliomalizika kule Misri, amecheza mechi 16 na kufunga bao moja tu na asisti moja vilevile akutika kwa dakika 943.
Karidioula anasifiwa kwa kumudu kucheza kama mshambuliaji wa kati na wingi zote mbili, japo rekodi yake ya kutumia akiwa Misri imemuangushwa kwa kilichoelezwa kukosa nafasi ya kutumika muda mrefu na aina ya wachezaji waliopo katika timu aliyotoka.
Inaelezwa kwamba Simba imempa mkataba wa miaka miwili nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 na atatambulishwa siku chache kabla ya kuanza kwa kambi mpya wa klabu hiyo kwa msimu ujao.