Tanzania inavyoweza kutengeneza mabilionea wengi, ushawishi duniani

Dar es Salaam. Ripoti ya Africa Wealth 2023, imebainisha kuwa Tanzania ina watu 2,400 tu ambao utajiri wao unazidi dola milioni moja, wakazi sita pekee wakiwa na zaidi ya dola milioni 100 huku Taifa hili la pili kiuchumi Afrika Mashariki likiwa na bilionea mmoja tu.

Idadi mamilionea nchini imeongezeka kwa asilimia 20 ndani ya kipindi cha miaka 10 lakini wachambuzi wa mambo wanaeleza kuwa ongezeko hilo linaweza kuwa kubwa zaidi iwapo kungekuwa na mkakati wa makusudi wa kukuza wawekezaji wakubwa wazawa, wanaoweza kupeleka bidhaa na huduma za Tanzania nje ya mipaka na kujenga ushawishi wa Taifa kimataifa.

Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanasema hali hii ni matokeo ya ukosefu wa sera za kimkakati za kuzipa nguvu kampuni kubwa zinazochochea ukuaji wa haraka na ushindani wa kikanda.

Wanaamini kuwa Tanzania inapaswa kuangalia mifano ya nchi kama Marekani na China ambazo zimejijengea nguvu kubwa kupitia ruzuku, misamaha ya kodi na dhamana za mikopo kwa kampuni za ndani.

“Wapo matajiri wengi ambao serikali ikiamua kuwaongeza pesa sawa na walionazo sasa au hata nusu yake wanaweza kufanya makubwa na pengine utegemezi wetu nje ya nchi utapungua,” anasema mfanyabiashara wa Dar es Salaam Amina Salum.

Anachokisema Salum kinatokea katika mataifa mengi. Mathalan serikali ya Marekani, inatumia kiasi kikubwa cha rasilimali kuhakikisha kampuni za ndani zinabaki kuwa nguzo ya uchumi na ushawishi wa taifa hilo. Kwa mwaka 2024 tu serikali ya nchi hiyo ilikuwa zaidi ya Dola za Marekani 180 kwa ajili ya ruzuku ya kampuni zao.

Takwimu zilizopo zinaonesha kupitia mfuko wa ustawi wa kampuni Marekani imekuwa ikitoa ruzuku, misamaha ya kodi na dhamana za mikopo tangu mwaka 1920 hadi sasa katika yale maeneo ya kimkakati.

Miongoni mwa kampuni zilizopata ruzuku kubwa zaidi ni Boeing, iliyopokea zaidi ya dola bilioni 15 kusaidia utafiti na maendeleo ya teknolojia za anga na ulinzi, Intel, iliyopata dola bilioni 8 za kujenga viwanda vya microchip, kampuni ya Amazon na nyingineo zikiwamo Tesla, ambayo ilipewa ruzuku ili kukuza magari ya umeme.

Hatua hizi zimechangia Marekani kuendelea kuwa kinara wa teknolojia duniani, huku zikitengeneza ajira milioni kwa raia wake na kuongeza mapato ya ndani kupitia kodi. Pia, kampuni hizo zimekuwa mabalozi wa kiuchumi wanaopeleka ushawishi wa Marekani katika kila kona ya dunia.

Mbali na Marekani, China nayo imekuwa na mkakati kabambe wa kufadhili kampuni zake ili zianzishe miradi mikubwa nje ya nchi. Serikali ya Beijing kupitia Benki ya Maendeleo ya China imekuwa ikitoa mikopo ya riba nafuu na ruzuku kwa kampuni kama China Communications Construction Company (CCCC) na China Railway Engineering Corporation yanayojenga miundombinu katika nchi nyingi za Afrika na Asia.

Nchi za nyingi zinapokuwa zinatekeleza miradi yake ya miundombinu kampuni hizi zimekuwa zabuni kwa sababu serikali yao iliwawezesha kuwa na mtaji mkubwa wa kuwekeza na kushindana kwenye soko. Mbinu hii imeifanya China kuongeza ushawishi wake Afrika na kujenga nguvu kubwa ya kiuchumi duniani.

Nadharia ya uwanja sawa wa ushindani

Kwa muda mrefu, Tanzania imekuwa ikiendesha sera ya kutoa “uwanja sawa wa ushindani” kwa wafanyabiashara wote bila kujali ukubwa au mchango wao wa kiuchumi. Wataalamu wanasema ingawa mfumo huu una nia njema ya kutovibagua vikundi, hauwezi kuleta matokeo ya kimaendeleo kwa kasi kama ilivyoshuhudiwa katika mataifa yaliyoendelea.

Ili kutengeneza matajiri na kuinua utajiri wa nchi Tanzania hiana budi kuanzisha mfumo wa kimkakati wa kusaidia kampuni ambazo zimeonesha uwezo wa kuzalisha ajira, kukuza mauzo ya nje na kuongeza kodi za serikali.

Mfumo huo unaweza kujumuisha, ruzuku za moja kwa moja za fedha taslimu, kwa kampuni zenye historia ya mafanikio, msamaha wa kodi kwa muda maalum, ili kupunguza gharama za uendeshaji na kukuza mtaji na dhamana za mikopo nafuu, zinazowezesha kampuni kupata mitaji mikubwa bila kubeba mzigo wa riba kubwa.

Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa Abel Kinyondo anasema upendeleo wa kimkakati kwa ajili ya malengo mahususi unaweza kufanya hata hapa na ukaleta matokeo chanya kama ilivyokuwa kwa mataifa mengine.

“Ukizungumzia Marekani na China utakuwa umeenda mbali sana, hapo tu Ethiopia wanatekeleza utaratibu huo na unawalipa kwenye usafiri wa anga, shirika lao ni miongoni mwa mashirika yanayofanya vizuri duniani lakini ni kwa sababu linapata upendeleo fulani,” anasema Profesa Kinyondo.

Anasema hata hapa nchi serikali inaweza ikaangalia sekta za kipaumbele ambazo zinaweza kuinua uchumi wa nchi kisha wakaangaliwa watu ambao tayari wamefanikiwa katika sekta hizo na kuwapa nguvu zaidi ili kuongeza matokeo na kukuza sekta.

“Muhimu katika hili ni kuhakikisha kunakuwa na usimamizi mzuri na weledi wa hali ya juu kwanza wanaopewa kipaumbele wawe ni watu ambao tayari ni magwiji na sababu za kuwapa ziwe thabiti tofauti na hapo watanufaika wasioweza kunufaisha nchi,” anasema Kinyondo.

Jambo lingine ambalo Profesa Kinyondo anashauri ni kuwa makini katika kutambua aina ya uwekezaji ambao utakuwa na athari kwa mapana lakini pia kufanya tathmini ya kina kabla ya kuamua.

Mchumi Mwingine, Profesa Dickson Pastory anasema hatua ya kuwezesha wafanyabiashara wa ndani inaweza kuwa hata na manufaa ya usalama wa taifa katika kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa na huduma muhimu ndani ya nchi.

“Kwa zile bidhaa na huduma muhimu mfumo wa namna hii unaweza ukatoa uhakika wa upatikanaji wake badala ya kutegemea usambazaji kutoka nje ya nchi lakini pia hatua hii inaweza kuongeza ushindani wa nchi jukwaa la kiuchumi duniani,” anasema Profesa Pastory ambaye ni Mhadhiri wa Chuo cha Usimamizi wa biashara (CBE).

Hata hivyo anasema tofauti na kutoa ruzuku njia nyingine inayoweza kuwa bora zaidi ni msamaha wa kodi akisema kwa mataifa yanayoendelea kutoa msaada wa kifedha kwa kampuni inaweza kuwa jambo gumu lakini kusamehe kodi inawezekana.
“Kwa kufanya hivyo mtaji wa mfanyabiashara husika unakua na unaweza kuongeza fursa za ajira lakini kwa biashara za ndani kukua hata Pato la Taifa (GDP) nalo linaongezeka,” anasema Profesa Pastory.

Pamoja na kwamba sio jambo linaloshikwa kidedea, mara kadhaa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekuwa ikieleza kuwa iko tayari kuwasaidia wajasiriamali nchini kupitia Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa ajili ya Mauzo Nje ya Nchi (ECGS) pamoja Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SME-CGS).

BoT imekuwa ikieleza kuwa lengo lake ni kuwezesha sekta binafsi wenye miradi mizuri kuweza kupata mitaji kutoka kwenye benki na taasisi za fedha zilizosajiliwa chini na Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha 2006, pale wanapokuwa na upungufu wa dhamana.

Juni 6, 2023 wakati wa changamoto ya Dola, Gavana Emmanuel Tutuba aliliambia Mwananchi kuwa serikali imechukua hatua ya kuhamasisha ununuzi wa bidhaa za ndani kwa zile zinazopatikana na kuongeza uzalishaji wa bidhaa kwa ajili ya matumizi ya ndani na mauzo nje ya nchi (import substitution).

Alisema Bodi ya Wakurugenzi ya BoT ikiongozwa na yeye mwenyewe ilitembelea maeneo ya kimkakati ambayo yanatazamwa kuongeza thamani ya mauzo ya Tanzania nje ya nchi hivyo kuongeza mapato ya fedha za kigeni.

“Bodi ikiongozwa na mimi mwenyewe Mwenyekiti tulitembelea maeneo ya kimkakati kama viwandani, maeneo ya uongezaji wa thamani ya madini na mashamba makubwa leo lilikuwa ni kuangalia mahitaji ya wawekezaji hao, nini wanahitaji kuongeza uzalishaji na mauzo ya nje, tulitaka kujua kama kuna eneo lolote hususani la kifedha wanahitaji tuwashike mkono,” alisema Tutuba.

Alisema lengo ni kuongeza uzalishaji wa ndani na thamani ya mauzo nje ya nchi hivyo BoT imefanya mipango ya kuwawezesha wenye uhitaji kupitia dhamana ya benki na viwango vitatofautiana kati ya bidhaa moja na nyingine.

“Mfano tulitembelea kiwanda cha sukari cha Bakhresa Bagamoyo akianza uzalishaji yule anapunguza naksi iliyokuwapo hivyo hatutumii tena fedha za kigeni kununua kiwango hicho cha sukari. Vilevile tulitembelea kiwanda cha kuchenjua dhahabu hicho kikianza kitakuwa kinatoa dhahabu kamili kwa asilimia 80 hivyo thamani ya mauzo itaongezeka,” alisema Tutuba.

Related Posts