Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dkt. Goodwill Wanga, ametoa mwaliko rasmi kwa wawekezaji kutoka Urusi kuwekeza nchini, hususan katika sekta ya uongezaji thamani wa madini ya urani.
Amesema hatua hiyo itaiwezesha Tanzania kunufaika na teknolojia ya kisasa, kukuza ajira, na kuimarisha uchumi wa taifa.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Taifa la Urusi yaliyofanyika kwenye Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba, Dkt. Wanga alieleza kuwa Urusi ni kinara katika matumizi ya teknolojia, hasa kwenye uchimbaji wa gesi na rasilimali nyingine. Kwa mujibu wake, uwekezaji wa nchi hiyo nchini Tanzania unaweza kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya viwanda na miundombinu ya kisasa.
“Urusi ina historia nzuri katika masuala ya nishati na teknolojia. Tunaamini kuwa ushirikiano wa aina hii utasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza sekta ya viwanda nchini, ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa vifaa vya kidijitali na simu janja,” alisema Dkt. Wanga.
Aidha, alibainisha kuwa Tanzania bado haijatumia kikamilifu raslimali zake za gesi asilia, na hivyo serikali inawakaribisha wawekezaji wa Urusi kuja kushirikiana katika kuendeleza sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi.
Alisisitiza kuwa serikali tayari imeweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji kwa kutoa vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi, hasa kwa wale watakaowekeza katika teknolojia ya kidijitali na uzalishaji wa simu za mkononi.
“Kiwanda cha kuunganisha simu za mkononi ni hatua ya kimkakati, hasa kwa sasa ambapo taifa linatekeleza mpango wake wa miaka kumi wa mageuzi ya kidijitali,” aliongeza.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Urusi nchini Tanzania, Nikita Rassokhih, alipendekeza Siku ya Urusi iendelee kuwa sehemu ya kudumu ya Maonesho ya Sabasaba ili kuimarisha mawasiliano ya kibiashara kati ya mataifa hayo mawili. Pia alisisitiza kuwa Urusi iko tayari kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.
Naye Lulu Mkude kutoka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), alithibitisha kuwa taasisi hiyo itaendelea kuhamasisha ushirikiano wa kimataifa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, akitaja kuwa Maonesho ya mwaka huu yamevutia zaidi ya washiriki 5,000 kutoka mataifa 23.
Ushirikiano huu unaoimarika kati ya Tanzania na Urusi unatajwa kuwa sehemu ya juhudi za taifa kujenga uchumi wa viwanda, unaojumuisha teknolojia, uboreshaji wa thamani ya malighafi, na uhamasishaji wa uwekezaji kutoka nje.