ALIYEKUWA Kocha wa Azam FC, Rachid Taoussi ameajiriwa na Klabu ya Kawbad Athletic Club Of Marrakech (KACM) itakayoshiriki Ligi Kuu Morocco msimu ujao 2025/26.
KACM iliyopanda Daraja kucheza Ligi Kuu Morocco msimu ujao, imemtambulisha rasmi kocha Taoussi kwa mkataba wa miaka miwili hadi mwaka 2027.
Taoussi ambaye ni raia wa Morocco ni miongoni mwa makocha wenye CV kubwa kwani ameshawahi pia kuzifundisha Wydad na Raja za jijini Casablanca.
Vilevile, amewahi kuwa kocha wa timu ya taifa ya Morocco kuanzia mwaka 2012 hadi 2013 na katika mechi mbili za kufuzu Kombe la Dunia ilizocheza dhidi ya Tanzania, moja alishinda na nyingine akapoteza kwa mabao 3-1, kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.
Akiwa na timu mbalimbali za Morocco, Taoussi amewahi kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo msimu wa 1988/1989 akiwa na AS FAR Rabat, pia ubingwa wa kombe la Throne akiwa na MAS Fes msimu wa 2010/11.