Kilolo. Katika juhudi za kuwawezesha vijana Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, wito umetolewa vijana kutambua athari za dawa za kulevya na kuacha kuzitumia hivyo kugeukia fursa za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri hiyo kwa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Hayo yameelezwa Julai 9, 2027 na mtaalamu wa masuala ya dawa za kulevya, Amosi Mkungile ambapo amewahimiza vijana hao kuzigeuza changamoto zinazowakabili kuwa fursa za maendeleo, huku akisisitiza vijana kutumia maarifa na rasilimali walizonazo kujiletea maendeleo endelevu.
”Ni muhimu kwa vijana kutambua kuwa changamoto ni sehemu ya maisha, lakini kwa kutumia maarifa na juhudi binafsi, wanaweza kuzigeuza kuwa fursa za mafanikio,” amesema Mkungile.
Katika semina hiyo, Ofisa wa Polisi kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Kilolo, Inspekta Gahe Mrisho ametoa onyo kali kwa vijana kuacha kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya, huku akieleza kuwa matumizi ya dawa hizo yamekuwa chanzo kikubwa cha ongezeko la kesi za ukatili wa kijinsia na uhalifu katika jamii.
”Matumizi ya dawa za kulevya siyo tu yanaharibu afya ya mtumiaji, bali pia yamekuwa chanzo cha migogoro na uhalifu katika jamii zetu. Tunawaomba vijana waachane na tabia hii hatarishi,” amesema Inspekta Mrisho.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Afya ya Uzazi kutoka Shirika la IOP Wilaya ya Kilolo, Belina Mhanga amewahimiza vijana kuzingatia afya ya uzazi na kupanga uzazi kwa uangalifu.
Mhanga ameeleza kuwa ongezeko la mimba za utotoni na uzazi usiopangwa limekuwa changamoto kubwa kwa maendeleo ya vijana.
”Ni muhimu kwa vijana kujielimisha kuhusu afya ya uzazi na kupanga uzazi kwa uangalifu ili kuepuka changamoto zinazoweza kuathiri maisha yao ya baadaye,” amesema Mhanga.
Ofisa Tarafa wa Mazombe, Wilaya ya Kilolo, Silvanus King’ung’e ametoa pongezi kwa waandaaji wa semina hiyo na kuwataka vijana kutumia maarifa waliyopata kujiletea maendeleo.
King’ung’e amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kutoa fursa mbalimbali kwa vijana na ni jukumu lao kuzitumia ipasavyo.

Mtaalamu wa masuala ya madawa ya kulevya kutoka Shirika la Ilula Orphans Program (IOP), Amosi Mkungile akizungumza na vijana waliojitokeza katika uwanja wa mpira uliopo Kata ya Ng’osi wilayani Kilolo mkoani Iringa. Picha na Christina Thobias
Baadhi ya vijana walioshiriki semina hiyo wameeleza kufurahishwa na elimu waliyoipata na kuahidi kuitumia kuboresha maisha yao.
Vijana hao wamesema ema kuwa semina hiyo imewafungua macho kuhusu madhara ya dawa za kulevya na umuhimu wa kupanga uzazi.
”Semina hii imetufungua macho kuhusu hatari za dawa za kulevya na umuhimu wa kupanga uzazi. Tutaenda kutumia elimu hii kuboresha maisha yetu,” amesema Ally Mbidule mmoja wa washiriki.
Shughuli hiyo pia iliambatana na bonanza la michezo ambapo timu mbalimbali kutoka Kata ya Ng’osi ziliweza kushindana, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha ushirikiano na mshikamano miongoni mwa vijana.