Wapinzani Kenya waungana kumkabili Ruto

Nairobi.  Wakati Serikali ya Kenya chini ya Rais William Ruto ikipitia misukosuko kutoka kwa wananchi wake, viongozi wa vyama vya upinzani wameungana ili kumkabili huku wakiapa kumwondoa madarakani kwenye uchaguzi ujao, mwaka 2027.

Wapinzani hao wameungana zikiwa zimepita siku chache tangu kufanyika kwa maandamano ya Sabasaba yaliyofanyika Julai 7, 2025 katika kaunti 17 nchini humo ambako watu 32 waliuawa.

Idadi hiyo inafanya jumla ya waliopoteza maisha kwenye maandamano kufikia 115 ndani ya mwaka mmoja.

Viongozi wa upinzani wameanzisha vuguvugu jipya la kisiasa linalofanana na mbinu za kihistoria za kiongozi wa ODM, Raila Odinga, zikiwa ni juhudi za kupinga utawala wa Serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais Ruto.

Muungano huo mpya, unaoitwa Upinzani Ulioungana, unajumuisha vyama sita vya siasa, Chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) cha aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, Wiper cha Kalonzo Musyoka, People’s Liberation Party (PLP) cha Martha Karua.

Vyama vingine ni Democratic Action Party (DAP-K) cha Eugene Wamalwa, Democratic Party (DP) kinachoongozwa na Justin Muturi na Chama cha Jubilee kinachowakilishwa na mwenyekiti taifa, Torome Saitoti pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Fred Matiang’i.

Kundi hili limefufua mbinu za kimapambano zilizowahi kuhusishwa na Odinga, ikiwamo ushawishi wa kimataifa, hatua za kisheria, taarifa za mara kwa mara kwa vyombo vya habari na mikutano ya hadhara ya kuwashitaki kwa wananchi wanaotuhumiwa kuhusika na ukatili.

Viongozi hawa wamekumbatia mbinu zote za upinzani zilizotumiwa na Odinga huko nyuma na kuongeza juhudi za kupunguza uhalali utawala wa Rais Ruto.

Kuanzia maandamano ya mitaani hadi kususia bidhaa na huduma, muungano unaoongozwa na Gachagua na Kalonzo unaonekana kufuata mkondo wa upinzani wa kisiasa wa miaka ya nyuma.

Katika hotuba yake, Jumatano iliyopita, Gachagua alisema upinzani utawasiliana na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuhusu kile walichokitaja kama uhalifu dhidi ya ubinadamu uliofanywa wakati wa maandamano ya hivi karibuni.

“Tutawaandika ICC na taasisi nyingine za kimataifa kurekodi unyama huu. Serikali hii imewageukia raia wake,” alisema  akitumia mbinu aliyowahi kutumia Odinga wakati wa ukandamizaji wa serikali uliokuwa na vurugu.

Mpango wa upinzani unajumuisha wito wa maandamano makubwa na kutoshirikiana na taasisi za Serikali kama alama kuu za mikakati ya Odinga.

Tayari maandamano yameikumba miji mbalimbali ya Mlima Kenya, Nairobi na maeneo mengine huku upinzani ukiwahimiza Wakenya kupinga kwa amani kile wanachokiita utawala batili.

“Sisi, Upinzani Ulioungana, kwa mshikamano na nguvu zote za maendeleo, tunatangaza kuwa imetosha. 2027 ni mbali sana. Hatutakubali siku nyingine ya mauaji yasiyodhibitiwa, wala wiki nyingine ya ukandamizaji wa kikoloni,” alisema Dk Mukhisa Kituyi Jumanne iliyopita kwa niaba ya muungano huo.

Lakini katika majibu yake, Rais Ruto alisema Jumatano iliyopita: “Wamesema hawatasubiri hadi 2027 kupiga kura. Kwamba wanapanga vurugu kuangusha serikali. Nawatakia heri. Hii ni nchi ya kidemokrasia, huwezi kupanga mapinduzi ya serikali.”

Kauli yake ilifuatiwa na onyo kutoka kwa washirika wa serikali, walioutuhumu upinzani kwa kuchochea machafuko na kutaka kuiletea nchi vurugu kwa njia zisizo halali. Walisisitiza kuwa, Katiba ya Kenya inatoa njia za kisheria za kubadilisha uongozi na kukemea mbinu zozote za nje ya katiba.

Upinzani pia umefufua mbinu ya kususia ya Odinga. Gachagua na washirika wake wametangaza kuwa watachapisha “orodha ya aibu” ya biashara zinazodaiwa kunufaika na upendeleo wa serikali.

“Tutakoma kutumia nguvu zetu za ununuzi kwa hawa wanaoshirikiana na utawala,” alisema Dk Kituyi.

Orodha hiyo, inayotarajiwa kukusanywa kupitia usaidizi wa wananchi, itawaalika raia kutaja kampuni zinazodhaniwa kuunga mkono utawala wa Kenya Kwanza.

Wakosoaji wa hatua hiyo wanaonya kuwa, huenda ikazidisha mivutano na kuwaathiri wafanyakazi wa kawaida, huku waungaji mkono wakisema ni njia halali ya upinzani wa kiuchumi.

Mbinu hii inafanana na harakati za National Resistance Movement (NRM) ya Odinga mwaka 2018, iliyolenga Safaricom, Brookside na mashirika mengine yaliyotajwa kuunga mkono serikali ya Uhuru Kenyatta.

Wakati huo, kama sasa, washirika wa serikali waliitaja kama hujuma ya kiuchumi.

Kiongozi wa wengi bungeni, Kimani Ichung’wah, alitaja mbinu mpya ya kususa kuwa ni, “hatari na kuharibu” na kuilinganisha na uporaji ulioonekana wakati wa maandamano ya hivi karibuni.

“Wanataka kuangusha uchumi ili wapate madaraka. Huo si uongozi ni uharibifu,” alisema.

Hata hivyo, upinzani unasema kuwa ni sera za kodi kupindukia, ukatili wa polisi, na ukosefu wa uwajibikaji katika utawala wa Ruto ndiyo vinavyohatarisha nchi.

Mbali na juhudi za hapa nchini, upinzani unatafuta msaada wa kimataifa. Mikutano ya diaspora tayari imezinduliwa Uingereza na Marekani, huku wajumbe kama Dk Matiang’i wakishirikiana na mashirika ya kiraia na ya haki za binadamu kimataifa.

Gachagua anatarajiwa kusafiri hadi Washington DC kwa mikutano na watunga sera, Wakenya waishio ughaibuni na taasisi za kimataifa. Mbinu hii inafanana na ushawishi wa kimataifa aliowahi kuutumia Odinga baada ya uchaguzi.

Lengo ni kuyainua masuala ya ndani hadi kwenye majukwaa ya kimataifa, kuyawasilisha kama matatizo ya utawala yenye umuhimu wa kimataifa.

Wakati hayo yakiendelea, Rais Ruto jana  alitoa onyo kali hadi sasa kufuatia wimbi la hivi karibuni la maandamano ya kupinga serikali, akitishia kutumia nguvu kali dhidi ya waandamanaji wanaohusika na uporaji na uharibifu wa mali.

Katika mwelekeo mpya wa kisiasa, Dk Ruto aliutuhumu upinzani kwa kupanga njama kuvuruga amani nchini humo za kuiangusha serikali yake, akiwatahadharisha wapinzani wake kuwa, mamlaka yatachukuliwa tu kupitia uchaguzi, si kwa maandamano ya mitaani.

Ruto alisema, serikali haitakubali vurugu kuharibu maendeleo yaliyopatikana kwa miaka mingi.

 Akilalamikia maandamano ya hivi karibuni kusababisha mali ya wananchi wasio na hatia kuchomwa moto, Dk Ruto alionya kuwa, “kila mtu atakayebainika kuhusika na fujo hizo atawekwa jela.”

“Na kwa viongozi wao, tunawafuata. Huwezi kufadhili vurugu halafu uende zako bila kuchukuliwa hatua. Hatutakuwa na taifa linalotawaliwa kwa vurugu. Na haitatokea nikiwa madarakani. Hatutaruhusu wahuni kuivuruga nchi hii,” alisema Rais Ruto alipokuwa akikagua miradi ya serikali eneo la Kilimani, Nairobi.

Kiongozi huyo wa Taifa la Kenya aliwaonya wanaolenga vituo vya polisi na maofisa wa usalama kuwa, hakuna taifa linaloweza kustawi chini ya vitisho vya vurugu na kukosekana kwa sheria. Alisema kushambulia maofisa wa usalama na vituo vya polisi ni sawa na “kutangaza vita.”

“Mtu yeyote anayeshambulia kituo cha polisi na kuwapiga maofisa wa polisi, hilo halikubaliki. Imetosha sasa. Nitailinda Jamhuri ya Kenya. Narudia tena, wanaoshambulia vituo vyetu vya usalama, ikiwamo polisi,  hiyo ni aina ya ugaidi,” aliongeza Rais.

Rais Ruto alisisitiza kuwa, jaribio lolote la kuiondoa serikali kwa kutumia vurugu halitafaulu.

“Ni lazima tuambiane ukweli. Je, vijana wote walikuwa wameajiriwa awali? Sasa mnataka kuanzisha vurugu. Viongozi hawa waliokosa mawazo sasa wanasema hawatasubiri hadi 2027, kwamba watachochea umma na kuiangusha serikali kupitia machafuko. Wajaribu waone, watajifunza kwa njia ngumu,” alisema.

“Kwa wale wanaopanga gizani, nawaambia wazi. Kama mna ndoto za kuongoza, andaeni sera zenu na mkutane nami kwenye uchaguzi mwaka wa 2027. Hakuna njia ya mkato, hakuna mlango wa nyuma,” alisisitiza Rais.

Related Posts