Ifakara. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara, Pilly Kitwana amewaagiza waratibu elimu kata na wakuu wa shule za sekondari kuhakikisha wanasimamia vizuri miradi ya maendeleo katika shule zao.
Kitwana ametoa agizo hilo leo Julai 10, 2025 alipofanya kikao na waratibu elimu kata na wakuu wa shule za sekondari za Serikali na binafsi zilizopo katika halmashauri hiyo, lengo likiwa kuwakumbusha majukumu na wajibu wao katika kusimamia miradi kwenye maeneo yao ya kazi.
“Kila mmoja atekeleze wajibu wake kama umeletewa miradi kwa taratibu na miongozo iliyopo tafadhali miradi hiyo ikamilike kwa wakati. Huu ni mwaka mpya wa fedha kuna fedha zitaletwa kwa ajili ya miradi, hakikisheni mnaisimamia vizuri,” amesema Kitwana.
Amewasisitiza waratibu hao kuhakikisha wanaongeza ufaulu na kuimarisha uhusiano mwema kazini.
Pamoja na kujadili suala la usimamizi wa mradi, pia Kitwana amesikiliza changamoto na kero mbalimbali za waratibu hao wa elimu.
Kwa upande wake, Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Mji Ifakara, Folkward Mchami amewataka waratibu elimu hao kuhakikisha halmashauri hiyo haina mwanafunzi hata mmoja atakayepata daraja la mwisho katika mtihani wa kidato cha nne utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu.

“Tuna mpango wa kufuta divisheni ziro katika kila shule, hivyo sisi kama waratibu wa elimu pia tunapaswa kusimamia walimu na ufundishaji wao tuhakikishe wanafunzi wote wanafaulu kwa kuondoa utoro mashuleni na kuhakikisha walimu wanafundisha vipindi vyote kwa weledi,” ameeleza Mchami.