Dar es Salaam. Wakati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akitoa maagizo kutafutwa suluhisho la msururu wa malori ili kuondoa malalamiko ya watumiaji wengine wa barabara, wadau wametoa mapendekezo ya kumaliza kadhia hiyo.
Akizungumza katika kikao na watendaji wa mamlaka na taasisi mbalimbali wakiwamo watu wa bandari, wasafirishaji, wamiliki wa bandari kavu, wakuu wa wilaya na vyombo vya usalama, Chalamila amesema uwapo wa foleni umeibua kelele kwa watumiaji wa barabara, wengi wakiitaja kuwa sababu ya kushindwa kufika kazini kwa wakati.
“Njia ya Temeke, Kigamboni, Mandela hali ni mbaya, njia hazipitiki. Kila unapokwenda unakuta malori yanepaki yakisubiri kutembea kwenda bandarini au kutoka, mjazano wa magari umeibua malalamiko makubwa watu wanaingia kazini saa tatu, saa nne, saa 4:30 ukiuliza wanasema kulikuwa na foleni,” amesema Chalamila katika kikao hicho leo Julai 11, 2025.
Kutokana na hayo ametaka kutafutwa suluhisho la muda mfupi na mrefu, ikiwamo kuhakikisha mifumo inafanya kazi kwa wakati ili mizigo ihudumiwe kwa haraka na malori yatoke.
Pia ameitaka sekta binafsi kuangalia namna ya kuwekeza katika ujenzi wa barabara za juu za kulipia ili kusaidia watu wa magari madogo wasikae katika foleni kwa muda mrefu.
Hii si mara ya kwanza Chalamila kuzungumzia foleni ya malori yanayoingia na kutoka bandarini. Aliwahi kutoa maagizo akitaka wilaya zote kudhibiti watu wanaoegesha magari barabara za dharura akieleza eneo hilo si la maegesho.
Amemtaka Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam kukaa kikao na watoa huduma wote wa usafirishaji, Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) ili kutafuta suluhisho la kudumu.
Akizungumzia suluhisho la hali hiyo, Meneja uhusiano wa kampuni ya DP World, Eltunu Mallania amependekeza kuwapo utaratibu wa barabara kwa ajili ya magari yanayokwenda bandarini.
Amesema DP World pekee katika gati wanazohudumia wanapakua kati ya magari 1,800 hadi 2,000 kwa siku ambayo yote yanakwenda kutumia barabara zilizopo.
Mkuu wa shughuli za uendeshaji wa kampuni ya Tanzania East Africa Getway Terminal Limited (TEAGTL), Donald Talawa amesema ni vyema kuongeza kasi ya upelekaji makontena katika Bandari ya Kwala kwa kutumia reli ili kuendana na malengo ya uwekezaji uliofanyika, kwani hiyo itasaidia malori mengi kuishia huko badala ya kuja katikatika ya jiji.
“Hii itasaidia kuhakikisha ukuaji wa uhudumiaji wa mizigo unaoshuhudiwa katika Bandari ya Dar es Salaam hauathiri shughuli za barabara zetu za nje,” amesema.
Katibu wa umoja wa wamiliki wa daladala Dar es Salaam (Darcoboa), Shifaya Lema amesema: “Malori ni mengi, katika barabara hii yanasababisha msongamano na kuathiri shughuli zetu, mkitumia reli kupeleka mizigo Kwala itasaidia kuondoa msongamano.”
Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tamstoa), Issa John ametaka kuwapo mkakati wa kuhakikisha bandari kavu zinajengwa kilomita nane kutoka mji ulipo ili kuondoa msongamano.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha waendeshaji wa bandari kavu, Meleck Shange amesema licha ya jitihada za kuboresha huduma wanazozifanya lakini kuna changamoto ya kukosa uhakika wa kuhudumu kwa muda mrefu kutokana na mikataba ya mwaka mmoja mmoja wanayopewa.
“Tunapata uoga wa kufanya uwekezaji wa muda mrefu kwa sababu tunapewa leseni ya mwaka mmoja, sasa mashine moja unaagiza kwa Dola 500,000 (zaidi ya bilioni moja)” amesema na kuongeza:
“Unawekeza hujui kuna leo na kesho, hii inaleta changamoto kwetu. Tunamatumaini tutaongezewa miaka ili watu wapate nguvu ya kuwekeza na kuwapo maeneo maalumu hii itasaidia kutengeneza nafasi bandarini.”
Edward Mpogolo, kwa niaba ya wakuu wa wilaya mkoani Dar es Salaam amesema wamepokea maagizo, yakiwamo ya kuhakikisha wanaondoa msongamano unaoweza kuzuilika katika maeneo yao kwa kushirikiana na wadau wote.