YANGA inaendelea na marekebisho kadhaa ya kiufundi kwenye kikosi chake kuelekea kwenye maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo, inaripotiwa kwamba wataweka kambi ya maandalizi nchini Rwanda wiki chache zijazo. Lakini habari mpya ni kwamba jina la Kocha kijana Mfaransa mwenye uzoefu na soka la Afrika limetua mezani kwao.
Kocha huyo ni Romain Folz (34) lakini sifa yake kubwa ikitajwa ni soka la kushambulia lenye pasi nyingi na mtu makini kazini. Kazi yake ya mwisho ilikuwa Msaidizi kwenye benchi la Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini mwaka jana. Habari ambazo Mwanaspoti imezipata ni kwamba Yanga wako kwenye mazungumzo na Kocha huyo miongoni mwa tageti zao kuchukua nafasi ya Miloud Hamdi aliyetimkia Ismailia ya Misri.
Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe amenukuliwa akitamba kwamba tayari wameshamalizana na kocha mmoja kijana na watamshusha muda wowote ingawa akaficha jina lake.
Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika cha Mwanaspoti; “Makubaliano na kocha Romain Folz kujiunga na Yanga yako karibu kukamilika. Kuna mazungumzo yanayoendelea kuhusu mkataba wa miaka miwili pamoja na chaguo la mwaka mmoja wa ziada. Kulikuwa na makocha wengine waliokuwa wanatazamwa, lakini klabu imeonyesha nia kubwa kwa Kocha Folz.”
Awali Yanga ilitajwa kuonyesha nia ya kumuajiri Kocha kijana na maarufu wa Afrika Kusini, Rulani Mokwena lakini badae dili hilo likashindikana.
Lakini katika wiki za hivikaribuni amekuwa akitajwa zaidi, kocha wa ASEC Mimosas, Julien Chevalier, ingawa yeye inaelezwa kuwa uongozi wake umempa ofa nzuri na mikakati mipya asalie kwenye timu hiyo kutengeneza mifumo imara zaidi ya vijana na kuimarisha malengo ya klabu hiyo kimataifa. Hivyo Yanga huenda wakamkosa, ingawa lolote linaweza kutokea.
“Yanga inaamini kuwa Folz anaweza kuipandisha zaidi na kuendana na mipango yao ambayo ni kucheza pia soka la kuvutia, kufanya vizuri zaidi katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao. Wana imani kuwa wana kikosi bora na kuwa na Romain Folz kama kocha kutawawezesha kwenda mbali zaidi kwenye mashindano hayo,” kilieleza chanzo chetu.
Folz amejijengea jina Barani Afrika baada ya kuifundisha Township Rollers ya Botswana, alihamia Afrika Kusini mwaka 2022 kujiunga na Marumo Gallants, ambapo alikua kocha mdogo zaidi katika Ligi Kuu wakati huo. Baadaye alihamia AmaZulu FC, kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo mwaka 2023.
Katika msimu wa 2024/25, alijiunga na Mamelodi Sundowns kama kocha msaidizi lakini aliacha kazi pamoja na kocha mkuu Manqoba Mngqithi, miezi michache baada ya msimu kuanza.
Kuzaliwa: Juni 28, 1990 (34)
Sehemu: Bordeaux, Ufaransa
2018-West Virginia United
2019–2020-Pyramids (Msaidizi)
2020–2021-Niort (Msaidizi)
2021–2022-Township Rollers
2024-Mamelodi Sundowns (Msaidizi)