HUKUMU MAUAJI YA MUUZA MADINI MTWARA:Kutoka mipango, mauaji mpaka kunyongwa askari Polisi – 12

Dar es Salaam. Katika sehemu hii ya simulizi ya hukumu ya kesi ya mauaji iliyokuwa ikiwakabili maofisa saba wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, Mahakama inafafanua majukumu ya kila mshtakiwa katika tukio hilo.

Washtakiwa hao katika kesi hii ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Mtwara (OC-CID), Mrakibu wa Polisi (SP) Gilibert Kalanje, na aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Onyango.

Wengine ni aliyekuwa Mkuu wa Intelijensia wa Wilaya ya Mtwara (DCIO), ASP Nicholous Kisinza, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Marco Chigingozi, Mkaguzi wa Polisi, John Msuya, Inspekta Msaidizi Shirazi Ally Mkupa na Koplo Salim Mbalu.

Wote walishtakiwa kwa kosa la kumuua kwa kukusudia mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamisi, mkazi wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi, Januari 5, 2022, ndani ya Kituo cha Polisi Mitengo, Wilaya ya Mtwara.

Jaji Hamidu Mwanga kutoka Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam anafafanua majukumu ya kila mshtakiwa hao na kujibu kiini cha pili cha shtaka, kama washtakiwa wanahusika na mauaji hayo au la, kama ifuatavyo:

Jaji Mwanga amerejea ushahidi wa mashahidi mbalimbali wa upande wa mashtaka, akiwemo shahidi wa tatu, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mtwara (RCO) wakati huo, sasa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Yustino Mgonja.

ACP Mgonja aliyetoa ushahidi kama shahidi wa tatu upande wa mashtaka, pamoja na mambo mengine alieleza kuwa Januari 5, 2022, alipokea barua kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka mkoa wa Mtwara (NPS) ikihusu malalamiko ya Mussa, aliyemtaka afanye uchunguzi wa malalamiko hayo.

Mussa aliwatuhumu baadhi ya askari wa Kituo cha Polisi Mtwara kwa kufanya upekuzi nyumbani kwake, Kijiji cha Luponda, na kuchukua mali zake.

Alieleza kuwa Oktoba 20, 2021, mshtakiwa wa tatu alipata taarifa kuwa watu wawili walikuwa wakitumia fedha kwa fujo kwenye nyumba ya kulala wageni ya Sadina. Alichukua hatua ya kumjulisha mshtakiwa wa kwanza, ambaye alipanga timu ya kwenda kuwakamata.

Siku hiyohiyo, mshtakiwa wa nne, wa sita, na wa saba chini ya usimamizi na maelekezo ya mshtakiwa wa kwanza, pili, na wa tatu, walimkamata Mussa na kuchukua pesa zake Sh2.3 milioni kutoka kwake.

Washtakiwa walimuweka kizuizini Mussa kwa njia isiyo halali kwa kutumia kumbukumbu ya kitabu (RB) ya kughushi, wakimtuhumu kwa wizi wa pikipiki, ilhali RB hiyo ilihusiana na kosa la uvunjaji nyumba na wizi.

Oktoba 21, 2021, mshtakiwa wa nne, sita, na saba walikwenda na Mussa nyumbani kwake Kijiji cha Luponda, Wilaya ya Nachingwea kufanya upekuzi, ambako walichukua fedha za kigeni (Dola za Marekani) pamoja na fedha za Kitanzania.

Walirudi Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara bila kufungua kesi yoyote dhidi ya Mussa, fedha zilizokamatwa zilikabidhiwa kwa mshtakiwa wa kwanza mbele ya mshtakiwa wa pili na wa tatu. Oktoba 24, 2021, Mussa alipewa dhamana.

Washtakiwa walithibitisha ushahidi wa Jamhuri

Watatu kati ya washtakiwa hao waliotoa ushahidi wao wa utetezi kama mashahidi namba 4, 6, na 7 walithibitisha jambo hili. Kama shahidi wa nne wa utetezi alivyoeleza, walipofika Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara, alimkabidhi vielelezo vilivyokamatwa kwa mshtakiwa wa kwanza mbele ya mshtakiwa wa pili.

“Kwa hiyo ushahidi unaonesha mshtakiwa wa nne, sita, na saba walimleta mtuhumiwa (Mussa) akiwa na afya njema na aliachiliwa kwa dhamana hadi mshtakiwa wa nne alipolekezwa na mshtakiwa wa kwanza kumtaka Mussa aripoti kwake,” alieleza Jaji Mwanga na kuongeza kuwa:

“Hivyo Mussa baada ya kuitwa alifika Kituo cha Polisi Mtwara Januari 5, 2025, akakutana na mshtakiwa wa kwanza ofisini kwake. Hiyo ndiyo ilikuwa nafasi ya washtakiwa wa tatu, nne, sita, na saba kulingana na ushahidi.”

Kwa mujibu wa Jaji Mwanga, kundi hili linamhusisha mshtakiwa wa tano, Inspekta Msuya, ambaye ni daktari wa Zahanati ya Polisi Mtwara.

Kulingana na shahidi wa tatu wa Jamhuri, ACP Mgonja, Januari 5, 2022, mshtakiwa wa kwanza alimweleza kuwa walikuwa na mwizi sugu wa pikipiki, lakini hakutaka kutoa taarifa za uhalifu wake na wenzake.

“Hivyo akamtaka awasaidie kumdunga sindano ya sumu mshatakiwa wa tano. Alikataa, akapendekeza kuwa kuna dawa ya kumpoteza fahamu, akizinduka atatoa taarifa kuhusu tuhuma zilizomkabili,” alieleza Jaji akichambua ushahidi.

“Mshtakiwa wa kwanza alikubali na kazi hiyo ilifanyika katika Kituo cha Polisi Mitengo. Mshtakiwa wa tano alimdunga Mussa sindano ya dawa ya Ketamine 1cc kwenye mshipa wa mkono wa kulia, mbele ya mshtakiwa wa kwanza, wa pili, na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Mahembe.”

Kundi la tatu la washtakiwa

Kundi hili linawahusisha washtakiwa wa kwanza na wa pili ambao walikuwa OC-CID na OCS mtawalia.

Kulingana na ushahidi, mshtakiwa wa kwanza ndiye aliyeteua timu ya kufanya upekuzi na ukamataji, na mshtakiwa wa pili alitoa amri na hati ya safari kwenda kijiji cha Luponda kufanya upekuzi.

“Mali zilizokamatwa zilikabidhiwa kwa washtakiwa wa kwanza na wa pili bila hati ya makabidhiano ya maandishi, na hakuna jalada la kesi lililofunguliwa. Mpaka sasa, mali hizo zimeendelea kuwa mikononi mwa washtakiwa hao.”

“Mchana siku hiyo hiyo, Januari 5, 2022, mshtakiwa wa kwanza, wa pili, Inspekta Msaidizi Mahembe, na marehemu Mussa walifika Kituo cha Polisi Mitengo.”

Mshtakiwa wa kwanza alitoa taarifa kwa shahidi wa 25 wa Jamhuri, Inspekta Paulo Kiula, aliyekuwa Mkuu wa Kituo hicho. Baadaye kidogo, shahidi huyo aliwaonesha ofisi ambamo wote waliingia pamoja na Mussa.

“Mshtakiwa wa kwanza alimwambia mshtakiwa wa tano kuwa huyo kijana ‘Mussa’ ambaye hakuwa na shati, akiwa amefungwa mikono nyuma, ndiye aliyepaswa kudungwa sindano. Mshtakiwa wa tano akamdunga sindano hiyo.”

“Mara mshtakiwa wa kwanza alisema: ‘Huyu anatuchelewesha,’ akachukua tambala akamziba Mussa pua na mdomo. Mshtakiwa wa tano alipoona hayo alitoka nje kwani sivyo walivyokuwa wamekubaliana.”

“Baadaye mshtakiwa wa kwanza, wa pili, na Inspekta Msaidizi Mahembe nao walitoka, mshtakiwa wa kwanza aliyekuwa na funguo akafunga mlango kwa kufuli, wakaondoka wote wanne,” alieleza Jaji katika uchambuzi huo.

Shahidi wa 23, Koplo Happy, alithibitisha kuwaona washtakiwa wa kwanza, wa pili, wa tano, Afande Mahembe, na Mussa, walipowasili kwa gari la kiraia katika Kituo cha Polisi cha Mitengo, Januari 5, 2022, kati ya saa 8 hadi 9 alasiri.

Kwa mujibu wa Jaji, shahidi huyo aliwaona wakiingia katika chumba, lakini mshtakiwa wa tano alitoka baada ya dakika 10.

Kulingana na shahidi wa 25, washtakiwa wa kwanza na wa pili waliwasili kituoni hapo na Mussa, na mshtakiwa wa kwanza aliomba chumba kwa ajili ya kumhoji. Walipatiwa chumba kilichotumika kama stoo. Pia baadaye aliomba kufuli na wakamfungia Mussa humo, kisha wakaondoka na funguo.

Kwa mujibu wa ACP Mgonja, baada ya kuenea uvumi kuwa Mussa ametoweka, mshtakiwa wa tano akaamua kufichua siri. Pia aliwataja mshtakiwa wa kwanza, wa pili, na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Mahembe.

Mahembe alikwenda kuonesha mwili wa Mussa ulikotupwa katika msitu wa Hiari.

Mshtakiwa wa tano pia alieleza kuwa mshtakiwa wa pili na Mahembe walikuwepo wakati mshtakiwa wa kwanza alipomziba Mussa pua na mdomo kumkosesha pumzi. Pia alieleza kuwa kabla ya tukio hilo, mshtakiwa wa kwanza alikuwa ameeleza nia yake ya kumuua Mussa kwa sumu.

Baada ya kubainisha ushiriki wa kila mshtakiwa, nini Jaji Mwanga alikiamua na kwa nini? Fuatilia sehemu inayofuata…

Related Posts