JKT Queens yabeba kipa Mashujaa

JKT Queens msimu huu ndiyo itaiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya CECAFA ya kufuzu Ligi ya Mabingwa kwa Wanawake na tayari imeanza maboresho kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo langoni.

JKT itashiriki michuano hiyo baada ya kuwa mabingwa wa ligi msimu huu. Hii inakuwa mara ya pili kwa timu hiyo baada ya mwaka 2023 kuibuka mabingwa wa CECAFA.

Taarifa zilizopatikana na Mwanaspoti ni JKT imemalizana na aliyekuwa kipa wa Mashujaa, Asha Mrisho kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Timu hiyo imemsajili kipa huyo baada ya kuonyesha kiwango bora msimu huu akiwa na Mashujaa na timu ya taifa, Twiga Stars.

“Dhumuni la viongozi ni kuleta ushindani kwenye kikosi, pia kuwapa nafasi mabinti wadogo kuonekana kimataifa. Asha ni kipa mzuri na kwa umri wake tunaamini atafanya makubwa,” ilisema taarifa hiyo.

“Naijath Abbas amekuwa na kiwango bora kwenye timu na timu ya taifa, amekuwa akicheza mfululizo bila kupumzika, kwa hiyo kuwa na kipa mwingine mwenye ubora itamsaidia kupata mapumziko.”

Kwa sasa Asha yupo Morocco kwenye majukumu ya timu ya taifa, Twiga Stars inayoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON).

Katika ligi, kipa huyo ameruhusu mabao 21 kwenye mechi 18 alizocheza akiisaidia timu hiyo kumaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi.

Mbali na kipa huyo, JKT inahusishwa pia na usajili wa beki wa kulia Asha Omary na Winifrida Castory kutoka Yanga Princess.

Related Posts