Uwekezaji wa Serikali ya Tanzania katika kuimarisha mifumo ya kukabiliana na majanga kupitia Kituo cha Ufuatiliaji wa Majanga na Tahadhari ya Mapema (Situation Room) umeanza kuzaa matunda, baada ya nchi mbalimbali za Afrika kuonesha kuvutiwa na namna kituo hicho kinavyofanya kazi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa wataalamu kutoka Ghana, Togo na Burkina Faso yanayofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Menejimenti ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali Hosea Ndagala, alisema kituo hicho kimeongeza uwezo wa nchi kuchakata taarifa za viashiria vya majanga na kutoa taarifa za viashiria vya majanga na kutoa tahadhari mapema kwa wananchi.
“Uendeshaji wa kituo hiki unahusisha wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za Serikali wanaoshirikiana kuchakata taarifa kwa pamoja, jambo linalosaidia kutoa tahadhari kwa wakati,” alisema Brigedia Jenerali Ndagala.
Mkurugenzi Msaidizi wa kituo hicho, Bi. Jane Kikunya, alisema wageni kutoka nchi hizo tatu wameonesha kuvutiwa na mfumo wa ufuatiliaji wa majanga unaohusisha hadi ngazi za vijiji, na wamepanga kuiga mfumo huo katika nchi zao ili kuimarisha usimamizi wa maafa.
“Wameonesha nia ya kuitumia mifumo waliyojifunza hapa kwenye nchi zao. Hili ni jambo kubwa kwa ushirikiano wa kikanda,” alieleza Kikunya.
Katika mafunzo hayo, washiriki walielezwa namna kituo hicho kinavyokusanya taarifa kutoka sekta mbalimbali kama hali ya hewa, maji, kilimo, na kijamii, kisha kuzichambua na kutoa taarifa rasmi kwa vyombo husika na kwa wananchi.
Miongoni mwa wageni, Simboou Akleso kutoka Togo alisema: “Tumekuja Tanzania kubadilishana uzoefu kwa sababu mnafanya vizuri. Tumeshuhudia kwa macho namna taarifa zinavyokusanywa, kuchakatwa na kuwasilishwa kwa wananchi.”