Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), imewataka wamiliki wa magari ya usafiri wa abiria na mizigo kuhakikisha wanawaajiri madereva na makondakta wenye uelewa kuhusu Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.
Wito huo umetolewa Julai 11, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo pamoja na Kamishna wa DCEA, Aretas Lyimo, wakati wakizungumza kuhusu ushirikiano wa taasisi hizo mbili katika kudhibiti uhalifu wa kusafirisha dawa za kulevya kupitia vyombo vya usafiri.
“Sheria inatutaka yeyote yule au chombo chochote kinachokamatwa kikiwa kinasafirisha dawa za kulevya kinataifishwa pamoja na wanaoendesha hilo gari dereva na kondakta,” amesema Kamishna Lyimo.
Amesema wanataka kutoa elimu kwa madereva, makondakta pamoja na wamiliki wa magari ili kuelewa hiyo sheria wanapokamatwa na dawa za kulevya katika vyombo vyao, wanahusika moja kwa moja kwa kupakia mzigo huo.
“Abiria aliyepakia huo mzigo atahusika lakini kondakta na dereva watahusishwa kwa sababu wao wameruhusu ubebaji wa dawa za kulevya,” amesema.
Lyimo amesema lengo ni kuelewa wanachokipakia katika magari yao ni kitu gani ili wasijikute wanapakia dawa za kulevya.
Pia, amesema elimu hiyo itawasaidia wamiliki kujua sheria ya ukamataji wa magari yao kwani kinahusika moja kwa moja kwa kuwa kielelezo namba moja kesi inapofikishwa mahakamani.
Ameongeza kuwa hiyo itahakikisha wamiliki wanaajiri madereva na makondakta wenye uadilifu na kuingia nao mikataba kuhakikisha hawatabeba dawa za kulevya kwenye vyombo vyao.
“Katika adhabu za usafirishaji wa dawa za kulevya msafirishaji anapata kifungo cha maisha kulingana na mzigo alioubeba au kifungo cha miaka 30 na chombo husika kinataifishwa,” amesema.
Kwa mujibu wa Lyimo wamiliki wakielewa hili badala ya kulalamika kutaifishiwa mali zao watahakikisha wanaajiri watu waadilifu na watakuwa wanawafuatilia mara kwa mara kuhakikisha hawabebi dawa za kukulevya.
Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo amesema wamiliki wasipofuata sheria mitaji yao itapotea kwani sheria zimewekwa kwa ajili ya kulinda jamii.
“Chombo kinachobainika kinatumika kusafirisha dawa za kulevya, kinataifishwa haijalishi kina thamani ya Sh700 milioni au hata Sh1 bilioni, mtaji wa mmiliki unapotea na kama chombo hicho kilikopeshwa benki, bado atalazimika kuendelea kulipa deni hilo,” amesema Saluo.
Amesema wanapotoa leseni kuna masharti ya vitu ambavyo havitakiwi kusafirishwa, dereva anayeajiriwa anatakiwa kuthibitishwa na Latra. Pia, mwajiri ajiulize misingi na utamaduni aliojiwekea kwa madereva wake.
Pia, amesema kuna sheria na kanuni zinamuelekeza kondakta endapo atakuwa na mashaka na mzigo unaowekwa kwenye buti la gari akague kabla ya kuwekea alama.
Naye, Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), Mustafa Mwalongo amesema elimu hiyo itasaidia kueleza kinachoshindikana kufanya ukaguzi kwenye mizigo ya abiria.
“Wakija kutoa elimu itakuwa vizuri kwa sababu itakuwa sehemu ya pekee kuwaeleza njia ya kufanya pamoja na kuwepo kwa askari wanaohusika na dawa za kulevya kukagua mizigo na mabegi ya watu wakiwa stendi,” amesema Mwalongo.
Amesema ni ngumu kwa kondakta kukagumua mzigo wa abiria bila kibali na hakuna sheria inayomruhusu kufanya hivyo endapo kutakuwa na askari wanaohusika na jambo hilo itasaidia.
Mohamed Mohamed, dereva wa basi, amesema kuwakamata wao na makondakta ni kuwaonea kwa madai kuwa ipo mizigo inayopakiwa kutoka ofisini kwao.
“Kuna magari mizigo inapakiwa ofisini dereva hajui chochote anachojua ni kupeleka sehemu husika kwa kuwa sio mkaguzi na kila ofisi ina utaratibu wake wa kupokea mizigo na wanaogopa kupakia mizigo njia kwa sababu ya dhamana,” amesema Mohamed.
Amesema kuna kampuni zinafuatilia mwenendo wa gari kila hatua ni ngumu kupakia mizigo ovyo hivyo wa kuhojiwa ni wale wanaopokea na kuingiza kwenye magari.