Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam leo Ijumaa Julai 11, 2025 imepanga kutoa uamuzi wa maombi ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu.
Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa na Jaji Elizabeth Mkwizu baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili katika shauri hilo.
Lissu amefungua shauri la maombi akipinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuahirisha usikilizwaji wa kesi ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni uliotolewa Juni 2, 2025.
Katika maombi hayo, Lissu anaiomba Mahakama Kuu iitishe jalada la kesi hiyo ya jinai ili ichunguze na kujiridhisha, pamoja na mambo mengine uhalali na usahihi wa mwenendo wa shauri hilo kwa tarehe hiyo.
Upande wa wajibu maombi umeweka pingamizi kuhusu maombi hayo ikiiomba mahakama iyatupilie mbali, huku ikibainisha sababu tatu.
Katika sababu hizo imedai maombi hayo yanakiuka kifungu cha 372(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinachozuia rufaa au mapitio dhidi ya uamuzi au amri ya mahakama isiyomaliza shauri la msingi.
Sababu nyingine ni kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza maombi hayo kwani moja ya mambo anayoyaomba mwombaji yanalenga kuifanya mahakama iangalie kama kifungu cha 188 cha sheria hiyo kinakiuka au hakikiuki Katiba.
Sababu ya tatu mjibu maombi anadai ni batili kwa kujumuisha mambo mengi tofauti kwa pamoja.
Jopo la mawakili wa Lissu limepinga sababu za pingamizi hilo likidai hazina mashiko na kwamba maombi hayo yako sawa, hayajakiuka sheria yoyote, wakisisitiza mahakama ina mamlaka ya kuyasikiliza.