Mahakama Kuu yatupa maombi ya Lissu

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imetupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, baada ya kukubali pingamizi la Jamhuri kuwa yako kinyume cha sheria.

Uamuzi huo umetolewa leo Ijumaa, Julai 11, 2025 na Jaji Elizabeth Mkwizu.

Jaji Mkwizu amesema maombi ya mapitio yaliyowasilishwa na Lissu mahakamani hapo yapo kinyume cha kifungu 372(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA). Kifungu hicho kinazuia amri au uamuzi usiohitimisha shauri kukatiwa rufaa au kuombewa kufanyiwa mapitio.

Lissu amefungua shauri la maombi mahakamani hapo, akipinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuahirisha usikilizwaji wa kesi ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni uliotolewa Juni 2, 2025.

Aliiomba Mahakama Kuu iitie jalada la kesi hiyo ya jinai ili ichunguze na kujiridhisha pamoja na mambo mengine, uhalali na usahihi wa mwenendo wa kesi hiyo kwa tarehe hiyo.

Upande wa wajibu maombi umeweka pingamizi kuhusu maombi hayo, ukiiomba mahakama iyatupilie mbali huku ukibainisha sababu tatu.

Katika sababu hizo, imedai maombi hayo yanakiuka kifungu cha 372(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinachozuia rufaa au mapitio dhidi ya uamuzi au amri ya mahakama isiyomaliza shauri la msingi.

Sababu nyingine ni kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza maombi hayo kwani moja ya mambo anayoyaomba mwombaji yanalenga kuifanya mahakama iangalie kama kifungu cha 188 cha sheria hiyo kinakiuka au hakikiuki Katiba.

Sababu ya tatu, mjibu maombi anadai ni kuwa maombi hayo ni batili kwa kujumuisha mambo mengi tofauti kwa pamoja.

Jopo la mawakili wa Lissu limepinga sababu za pingamizi hilo likidai hazina mashiko, na kwamba maombi hayo yako sawa, hayajakiuka sheria yoyote, wakisisitiza mahakama ina mamlaka ya kuyasikiliza.

Related Posts