Makamu wa Rais apongeza ukaribu wa benki ya NMB na serikali

 Arusha.

Makamu wa Rais Dr Philip Mpango ameipongeza benki ya NMB kwa jinsi inavyoshirikiana na serikali katika matukio mbalimbali ya kijamii na kiuchumi nchini.

Amesema  kuwa kumekuwepo na mafanikio makubwa yaliyochagizwa na benki hiyo hasa katika kuhudumia jamii na kuwezesha shughuli  na matukio mbalimbali zinazofanywa na serikali.

“Kila ninapoiona benki ya NMB ikishiriki katika matukio mbalimbali ambayo serikali inaandaa kama mshirika wa karibu roho yangu inasuuzika kwa sababu najua kazi wanazofanya na uwezo walionao” amesema Dr Mpango.

Dr Mapango ameyasema hayo julai 10, 2025 jijini Arusha alipotembelea banda la maonyesho la NMB kabla ya kufungua mkutano wa 14 la watunga sera wa sekta ya mifuko ya hifadhi ya jamii Afrika uliofanyika katika ukumbi wa AICC.

Dr Mpango ametumia nafasi hiyo kuitaka Benki ya NMB kuhakikisha wanawekeza zaidi miundombinu ya benki hiyo hasa vijijini ili kutoa fursa kwa wananchi hao kupata huduma wanazotoa mijini kwa usawa.

Akitoa taarifa ya huduma wanazotoa, meneja wa kanda ya kaskazini kutoka Benki ya NMB, Baraka Ladislaus amesema kuwa benki hiyo imekuwa ikitenga fedha asilimia moja ya faida na kurejesha kwa jamii ili kusaidia serikali katika Nyanja mbalimbali.

“Kwa mwaka huu tumetenga zaidi ya shilingi  6.4 bilioni kwa ajili ya kuhudumia jamii hasa sekta ya Afya, Elimu na mazingira. Lengo ikiwa ni kurejesha faida kwa jamii inayotuzunguka lakini pia kuisaidia serikali katika kuhudumia jamii” amesema.

Mbali na hilo, Baraka amesema kuwa, kwasasa wana kampeni kubwa ya kuunga mkono kazi zinazofanywa na mifuko ya jamii kwenye kuimarisha uchumi wa wanachama, kuondoa umaskini na kupunguza utegemezi kwa jamii.

“Na sisi kama NMB tunazo bidhaa za kuunga mkono juhudi hizo ikiwemo ya ‘NMB Hekima plan’ ambayo inalenga watumishi waliostaafu na wale wanaotarajia kustaafu”

Amesema katika mpango huo wanatoa elimu mbalimbali kwa wahusika ikiwemo ya uwekezaji na utunzaji wa mafao  wanayoyapata ili yaweze kuendelea kuwapa tija na uendelevu.

“Lakini pia tunayo mpango maalum wa kujiwekea akiba kwa  muda ambao wateja wanajichagulia iitwayo ‘NMB jiwekee’, inayotoa fursa kwa wateja kuchagua kiwango cha kukatwa kutoka kwenye akaunti yake iwekwe kwenye akiba” amesema.

Awali akizungumzia mkutano huo, Waziri wa nchi, ofisi ya waziri Mkuu kazi vijana Ajira na wenye ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema kuwa mkutano huo umekutanisha wadau na watunga sera wa mifuko ya hifadhi ya jamii Afrika kwa lengo la kujadili hatma ya bara hili katika sekta ya miundombinu.

“Hapa wanajadili jinsi gani mifuko ya jamii Afrika inaweza kutengeneza utaratibu wao wa kuona jinsi ya kusaidia kutunisha mifuko ya ujenzi wa miundo mbinu katika bara la Afrika ili kukabiliana na ugumu wa upatikanaji wa fedha kutoka nchi zilizoendelea kutokana na migogoro ya kisiasa, mishtuko ya kiuchumi duniani na kupungua kwa ukuaji wa uchumi wa dunia”amesema.


Related Posts