….,……
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, leo Julai 11. 2025 amezindua zoezi la ugawaji wa mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.
Uzinduzi huo umefanyika katika viwanja vya stendi ya zamani mjini Katesh, wilaya ya Hanang, ambapo jumla ya mitungi 3,000 iliyokamilika na vifaa vyake imetolewa kwa wananchi kwa bei nafuu ya ruzuku ya shilingi 17,500 (elfu kumi na saba na mia tano) kwa kila mtungi. Aidha, imeelezwa kwa mkoa mzima wa Manyara jumla mitungi 16,275 itasambazwa na kuuzwa kwa bei ya ruzuku.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mheshimiwa Sendiga amesema mpango huo umelenga kuhakikisha wananchi wote, hususani wa kipato cha chini, wanapata fursa ya kutumia nishati safi na salama ya kupikia kwa gharama nafuu.
Aidha, amewaagiza Wakuu wa Wilaya wote mkoani Manyara kusimamia kwa makini zoezi hili, ili kuhakikisha mitungi hiyo inauzwa kwa bei iliyokubaliwa na kuepuka udanganyifu wa baadhi ya Mawakala/wafanyabiashara wasio waaminifu.
“Natoa rai kwa wakuu wa wilaya wote kuhakikisha utaratibu unazingatiwa, na mitungi hii inawafikia walengwa kwa bei ya shilingi 17,500 kama ilivyopangwa. Hatutavumilia wafanyabiashara watakaojaribu kulangua na kuuza kwa bei ya juu ili kujipatia faida isiyo halali,” amesema Sendiga kwa msisitizo.
Sendiga ameeleza kuwa kampeni hii ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inahoongozwa na Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan za kupunguza uharibifu wa mazingira unaosababishwa na ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa, na pia kulinda afya ya wananchi dhidi ya moshi unaosababisha magonjwa ya njia ya hewa.
Mpango huu wa ruzuku unatarajiwa kupunguza mzigo wa gharama ya awali kwa wananchi ya kununua majiko ya gesi na hivyo kuwa chachu ya mabadiliko kuelekea upishi salama na rafiki kwa mazingira.