Dar es Salaam. Jeshi la Polisi mkoani Tabora linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Castory Madembwe, mtumishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), mkazi wa Ipuli.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kutekeleza mauaji ya Madembwe, kisha kuufukia mwili wake nyuma ya nyumba inayodaiwa kupangishwa na mmoja wao, na juu ya kaburi hilo wakapanda zao la nyanya ili kuficha ushahidi.
Kabla ya taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa leo, Julai 11, 2025, Madembwe alikuwa hajulikani aliko kwa zaidi ya mwezi mmoja tangu kuripotiwa kutoweka, hali iliyozua sintofahamu miongoni mwa ndugu na marafiki. Mwili wake umepatikana ukiwa umezikwa kwa siri.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi mkoani Tabora, mama mzazi wa marehemu aliripoti kutoweka kwa mwanawe katika Kituo cha Polisi Tabora, Juni 12, 2025, akieleza kuwa hakuwa ameonekana tangu Juni 10, 2025.
Julai 9, 2025, Jeshi la Polisi mkoani humo lilitangaza kuwa lilimkamata Nelson Samwel akiwa na simu ya marehemu Madembwe.
Baada ya kuhojiwa, alikubali kuonyesha eneo walipoufukia mwili wa Madembwe, ndipo hatua za kisheria na kitaalamu zikachukuliwa ili kuufukua mwili huo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Inadaiwa kuwa licha ya kumuua Madembwe, watuhumiwa hao walimpigia simu mama mzazi wa marehemu wakidai kwamba mtoto wake ametekwa, na kumshinikiza atume fedha ili aachiliwe.
Kabla ya kukamatwa kwao, mama huyo alikuwa ameshatuma Sh5 milioni kama fidia ya kutaka kuokoa maisha ya mwanawe.
“Watuhumiwa hao ni Nelson Samwel, mkazi wa Ipuli Tabora (huyu ndiye mpangaji wa nyumba ambayo mwili huo ulifukiwa), Salum Heri, mkazi wa Kadinya, Bathoromeo Maiko, mkazi wa Isevya, Juma Ramadhani, mkazi wa Kidatu na Mohamed Hamad, mkazi wa Uledi,” taarifa ya Polisi imewataja hao miongoni mwa watuhumiwa wanaoshikiliwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, mtuhumiwa Careen Matemba, ambaye ni mke wa Nelson Samwel, bado anatafutwa baada ya kutoroka alipobaini wenzake wamekamatwa.
“Jeshi la Polisi linaendelea kutoa onyo kwa watu wengine wenye tabia kama hizi kuziacha, kwani lazima ipo siku watakamatwa. Kwa sababu ni suala la muda, hata kama kesi itachukua muda gani kuipeleleza, ipo siku mkono wa Dola utawafikia,” imeeleza taarifa ya Polisi.
Mkoa wa Tabora umekumbwa na msururu wa matukio ya mauaji na watu kujitoa uhai, likiwemo tukio la mama aliyeua watoto wake wanne kwa kuwalisha sumu, na kisha naye kunywa sumu hiyo, chanzo kikiwa inadaiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, tukio hilo lilimhusisha, Kang’wa Mahigi (25), mkazi wa Kitongoji cha Lugubu, Wilaya ya Igunga.
Inadaiwa alitumia sumu aina ya Ruruka 80WDG kuwapa watoto wake wanne kabla ya kujiua kwa kunywa sumu hiyo hiyo.
Watoto waliopoteza maisha wametajwa kuwa ni Sengi James (8), Simon James (6), Elisha James (3) na Kashinje James (miezi 7).
Katika tukio lingine, Jeshi la Polisi limesema mwanamke mwenye umri wa miaka 21 alijiua kwa kunywa sumu ya kuulia wadudu katika Kata ya Kalunde, Manispaa ya Tabora.