KIUNGO mkabaji wa zamani wa Simba, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar, Nassor Kapama licha ya kushindwa kuibakisha timu yake anatajwa kujiunga na Tabora United kwa ajili ya msimu ujao 2025/26.
Kapama ambaye alirejea Kagera Sugar akitokea Mtibwa Sugar amemaliza mkataba wake na waajiri wake hao hivyo ataondoka akiwa mchezaji huru.
Chanzo cha kuaminika kutoka kwa rafiki wa karibu wa mchezaji huyo kimeliambia Mwanaspoti ni kweli kiungo huyo yupo mawindoni na Tabora United ambayo imeonyesha nia ya kumsainisha ili kuongeza nguvu kikosini mwao msimu ujao.
“Taarifa nilizonazo, Kapama yupo kwenye hatua nzuri za kukamilisha usajili na Tabora licha ya kwamba nyota huyo ana ofa nyingi mbali na timu hiyo Mbeya City pia wamemtumia ofa ili aweze kuungana nayo mara baada ya kupanda daraja,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
“Licha ya Mbeya City kuonyesha nia kiungo huyo ameridhishwa na ofa nzuri ya mwaka mmoja aliyowekewa na Tabora United hivyo naamini ni suala la muda tu kuhusu Kapama kupata timu ya kuitumikia msimu ujao.”
Mwanaspoti lilifanya jitihata za kumtafuta Kapama ambaye alisema ni kweli sasa ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na Kagera Sugar ambayo imeshuka daraja msimu huu.
“Ni mchezaji huru na tayari nina ofa tatu mkononi mbili za ligi kuu na moja kutoka Uturuki siwezi kuzungumzia kwa sasa hadi hapo nitakapomalizana na moja kati ya timu hizo,” alisema na kuongeza;
“Siwezi kuzungumzia taarifa ambazo bado hazijakamilika, ninachoweza kusema ni kweli nimepokea ofa kutoka katika timu mbili za ligi kuu na moja kutoka uturuki kuziweka wazi sio sahihi lakini mambo yakienda vizuri kila kitu kitawekwa wazi.”