Nickson Kibabage kumfuata Kijili Singida Black Stars

BEKI wa zamani wa Yanga, Nickson Kibabage ambaye amemaliza mkataba na timu hiyo aliyoitumikia kwa miaka miwili anatajwa kurejea kwa waajiri wake wa zamani Singida Black Stars iliyomnyakua beki wa kulia wa Simba, Kelvin Kijili.

Kibabage alijiunga na Yanga kwa mkopo wa miezi sita na baadae kumnunua mazima kwa mkataba wa miaka miwili ambayo imetamatika mwisho wa msimu huu.

Chanzo cha kuaminika kutoka Yanga kililiambia Mwanaspoti, Kibabage hatakuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo msimu ujao na wapo kwenye mchakato wa kutafuta beki mzawa ambaye atasaidiana na Chadrack Boka.

“Yanga imeingia sokoni inatafuta beki mzawa ambaye atasaidiana na Boka upande huo, kuhusu Kibabage hatakuwa sehemu ya kikosi chetu msimu ujao amemaliza mkataba na sisi,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;

“Boka hayupo timamu licha ya kuwa na ubora hivyo anahitaji msaidizi ambaye watagawana mechi ukiangalia tuna mashindano mengi msimu ujao ligi ya ndani, Kombe la Shirikisho (FA) na Ligi ya Mabingwa Afrika.”

Wakati Yanga wakifunguka hayo Mwanaspoti linafahamu beki huyo anatajwa kurudi Singida BS ambayo ameitumikia kwa msimu mmoja na nusu.

Chanzo kutoka Singida BS kililiambia Mwanaspoti wanafanya makubaliano na beki huyo kwa ajili ya kumsainisha mkataba mpya ili arudi kuitumikia timu hiyo.

“Ni kweli kuna mazungumzo baina yetu na mchezaji huyo japo ni mapema sana kuzungumzia hilo mambo yakiwa tayari kila kitu kitawekwa wazi kwa sababu timu sasa ipo chini ya kocha mpya ambaye pia ana mipango yake na usajili anaoutaka.”

Uwepo wa Kocha Miguel Gamondi ndani ya kikosi cha Singida BS ni fursa kwa beki huyo, kwani alikuwa chaguo la kwanza chini yake akimtupa benchi Kibwana Shomari.

Mbali na kucheza kama beki, Kibabage pia amekuwa akitumika kama winga kwenye baadhi ya michezo kuanzia akiwa Mtibwa. Kabla ya kujiunga na Singida kwenye dirisha dogo beki huyo aliwahi kukipiga Mtibwa Sugar, KMC na Difaa Al Jadida ya Morocco.

Related Posts