Dar es Salaam. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa nchini (Nida) imesema inaandaa mkakati wa kufanya utafiti ili kuanza kutoa vitambulisho vya taifa kwa watoto nchini.
Hayo yamebainishwa na Ofisa Uhusiano wa Nida, Godfrey Tengeneza, alipozungumza na Mwananchi leo Ijumaa, Julai 11, 2025.
Tengeneza amesema mamlaka hiyo imejipanga na ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu ili kujua changamoto na namna ya kuziepuka katika uendeshaji wa zoezi hilo.
Akizungumzia utafiti unaokusudiwa kufanywa, ofisa uhusiano huyo ameweka wazi kuwa Nida inatarajia kufanya majaribio katika maeneo machache yaliyoainishwa ili kupata njia sahihi ya kutekeleza, lengo likiwa ni kuhakikisha huduma ya vitambulisho vya taifa inawafikia Watanzania wa makundi yote.
“Tunatarajia kufanya majaribio katika wilaya kadhaa ambazo mamlaka imezichagua. Baada ya utafiti huo, ambao utatupa picha halisi ya changamoto na namna ya kuziepuka, mamlaka itatangaza rasmi tarehe ya kuanza kusajili na kutoa vitambulisho vya taifa kwa watoto nchini,” amesema.
Akitaja maeneo yanayokusudiwa, Tengeneza amebainisha kuwa takribani wilaya tatu zitahusika katika majaribio hayo, zikiwemo Rungwe mkoani Mbeya pamoja na Unguja visiwani Zanzibar.
Amesema matarajio ya mamlaka hiyo ni kukamilisha mchakato huo mapema hadi kufikia mwanzoni mwa Agosti 2025, huduma zianze kutolewa.
Hatua hii inakuja takribani miezi mitatu tangu mamlaka hiyo ilipotoa taarifa juu ya uamuzi wake wa kuwafikia watoto katika utoaji wa vitambulisho hivyo, hatua iliyotajwa kuwa ni agizo la Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Jumatatu, Aprili 14, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa Nida, James Kaji, alisema agizo la Rais ni kuhakikisha Nida inayafikia makundi yote nchini huku ikitoa huduma kwa ufanisi.
“Hitaji la Rais Samia ni kuona mamlaka inatanua wigo wa huduma zake kwa kuyafikia makundi mbalimbali, wakiwemo watoto, ili kuondoa usumbufu wanaopata katika kuhitaji huduma mbalimbali,” alisema.
Mkurugenzi huyo aliweka wazi kuwa wananchi wamekuwa wakipata usumbufu katika kupata huduma, hivyo mamlaka imejipanga kuboresha mazingira ili huduma zipatikane kwa urahisi na kwa ubora unaostahili.