Baada ya kocha wa Twiga Stars Bakari Shime kusema kuwa walipoteza mchezo uliopita wa Kombe la Mataifa Afrika kwa Wanawake (WAFCON) kutokana na kuwakosa baadhi ya mastaa wake, leo mshambuliaji Opah Clement atakuwa uwanjani.
Twiga Stars inaingia uwanjani leo kuvaana na Afrika Kusini ambayo ndiyo mabingwa watetezi wa michuano hiyo, ilianza kwa kuchapwa bao 1-0 na Mali katika mechi ya kwanza ya Kundi C iliyopigwa Jumatatu iliyopita na leo inashuka kwenye Uwanja wa d’Honneur d’Oujda kuanzia saa 4:00 usiku kusahihisha makosa mbele ya watetezi walioanza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ghana.
Ujio wa Opah Clement, aliyekosekana mchezo uliopita kutokana na kadi tatu za njano, utaongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji ambalo lilikosa utulivu kwani ni mshambuliaji mwenye nguvu na maamuzi langoni mwa wapinzani.
Twiga inahitaji ushindi mbele ya Banyana Banyana ili kuweka hai matumaini ya kuvuka makundi kwenda hatua ya robo fainali kwani kipigo chochote kitaiweka pabaya ikiwa tayari wapinzani wao wana pointi tatu sawa na Mali ambayo mapema saa 1:00 usiku itavaana na Ghana inayoburuza mkia.
Lakini hata droo inaweza kuwa nafuu kwa Twiga huku ikisikilizia matokeo ya timu kutoka makundi mengine kuangalia namna ya kupenya kupitia Best Looser kwani itaifanya kupata pointi moja ikibakiza mchezo wa mwisho hatua ya makundi dhidi ya Ghana.
Kabla ya mechi za jana za michuano hiyo inayofanyika nchini Morocco, Twiga Stars ilikuwa nafasi ya pili kwa upande wa timu mbili zinazonyemelea kupitia mlango wa Best Looser ili kufuzu robo fainali, nyuma ya Senegal iliyocheza mechi mbili na kukusanya pointi tatu, huku Botswana ambayo jana ilikabiliana na Nigeria, ikiwa ya tatu na haina pointi, hivyo sare hiyo inaweza kuwasogeze juu zaidi.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kanuni za kupata nafasi ya kufuzu robo fainali ya michuano hiyo kupitia Best Looser, kigezo cha kwanza kinaangaliwa ni idadi ya pointi, ikiwa sawa inaangaliwa tofauti ya mabao, kisha mabao yaliyofungwa, kipengele cha nne ni nidhamu na mwisho kabisa ni kupiga kura. Kumbuka michuano hiyo ina makundi matatu, huku timu mbili za juu kila kundi zitafuzu robo fainali, kisha mbili za Best Looser zitaungana nazo kukamilisha idadi ya timu nane.
Hata hivyo, mechi hiyo si rahisi kwa Twiga Stars kutokana na rekodi ya Afrika Kusini, iliyocheza Kombe la Dunia mara mbili na mara ya mwisho ilikuwa ni 2023 ilipoishia 16 Bora.
Banyana Banyana ambayo ikishinda mchezo huu itakuwa imeshafuzu robo fainali, inapenda kushambulia kwa idadi kubwa ya wachezaji, hasa kupitia mawinga, hivyo huacha nafasi kubwa nyuma kupitia mabeki wa pembeni. Kama Twiga Stars itashambulia kwa kushtukiza mara kwa mara, itawachanganya wapinzani.
Akizungumza kuelekea mchezo huo Shime alisema wanafahamu ugumu wa mchezo huo, hivyo wamejiandaa kuhakikisha makosa waliyofanya mchezo uliopita hayajirudii.
“Tulitengeneza nafasi nyingi mechi iliyopita, tulikuwa na nafasi nzuri ya kufunga mabao lakini hayo tumeyaacha na tumeelekezana kuelekea mechi na Afrika Kusini. Tunaamini tutafanya vizuri.”