Mbeya. Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya, limetangaza oparesheni maalumu ya kubaini wamiliki wa shule ambao wanakwepa kupeleka mabasi yanayosafirisha wanafunzi kukaguliwa.
Hatua hiyo imetokana na mwamko mdogo wa baadhi ya shule kukiuka sheria sambamba na kutumia daladala za umma kusafirisha wanafunzi bila kibali.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Julai 10, 2025 Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya (RTO), Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, SSP Notker Kilewa, baada ya kuhojiwa kuhusiana na changamoto za ubovu wa mabasi yanayotumika kusafirisha wanafunzi hususani kukodi daladala za abiria, amesema kuwa kumekuwepo na kasumba ya baadhi ya wamiliki au wakuu wa shule kukwepa zoezi la ukaguzi wa mabasi ya wanafunzi na kudiliki kutumia mabasi ya umma yasiyo na kibali.
“Tutafanya msako mkali na kwenye Shule zote mkoani hapa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (Latra ) ili kubaini wanao kwepa kutekeleza takwa la kisheria la kufanyiwa ukaguzi kila muhula shule zikifunguliwa,” amesema.
Amesema katika msako huo shule ambazo zitabainika mabasi ya wanafunzi kutumika bila ukaguzi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi sambamba na kutozwa faini.
Kuhusu mabasi ya abiria kutumika kusafirisha wanafunzi, Kilewa amesema awali zipo baadhi ya shule ambazo hazina magari ya kutosha waliomba vibali ambavyo mwisho wa kutumika ni Julai mwaka huu.
Katika hatua nyingine amewataka madereza kuwafichua wamiliki wa vyombo vya moto wanaoshindwa kufanyia matengenezo kwa maslai yao binafsi.
Katika hatua nyingine amesema wameweza kufanikiwa kwenye matumizi ya Mfumo wa Vithibiti Mwendo wa Mabasi (VTS) ,ambapo kwa kwa siku mabasi 30 ukamatwa yakiuka sheria za barabarani.
“Nionye madereva kutii sheria bila shuruti lakini pia toeni taariza za wamiliki wanawapa vyombo vya moto vibovu kuingiza barabara ili tuweze kufanyia kazi na kuhepuka ajali zisizo za lazima,” amesema.
Kauli za wananchi, wazazi
Ester Damian Mkazi wa Uyole jijini hapa, amesema kumekuwa na kasumba kwa baadhi ya shule kutumia mabasi ya abiria kusafirisha wanafunzi na kuchukua idadi kubwa jambo ambalo ni hatari.
“Tabia hiyo imeota mizizi unakuta watoto watano wamekaa kwenye kiti ambacho wanatakiwa kukaa watu watatu, lakini wao waangalia pesa badala ya uhai wa watoto wanaosafirishwa,”amesema
Macha amesema jambo lingine ni matumizi ya mabasi yasiyokuwa na rangi na mkanda unatambulisha ni basi la wanafunzi na kuomba Jeshi la Polisi kulifanyia kazi.
Mmoja wa Walimu ambaye hakutaka jina lake kutajwe, amekiri kuwepo kwa changamoto ya usalama mdogo wa mabasi yanayo safirisha wanafunzi.