Dar/Mikoani. “Ninaweza kumwelezea Qares (Mateo) kama mmoja wa watu wakweli. Alikuwa na kiwango cha chini sana cha unafiki na hakuogopa kusema kile anachofikiri. Ni watu wachache wanaoweza kusema jambo hata kama halimpendezi mtu, lakini akalisema kwa uwazi.”
Ni kauli ya mwanasiasa mkongwe nchini, Jenerali Ulimwengu, akimwelezea Qares, aliyefariki dunia Julai 9, 2025, saa 4:00 usiku katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH). Anatarajiwa kuzikwa Jumatatu, Julai 14, 2025, eneo la Nakwa, Kata ya Bagara, wilayani Babati, mkoani Manyara.
Jenerali, akizungumza na Mwananchi leo, Julai 11, 2025, amesema Qares alikuwa mkweli, mwenye msimamo na asiyeyumbishwa. Daima alisimamia alichokiamini, sifa anayosema wanayo watu wachache, hasa kwa nyakati za sasa.
“Ni sifa kubwa. Wakati ule watu walikuwa wanajifanya hawaoni mambo ambayo yako wazi, lakini kwa sasa ni sifa kubwa zaidi kwa sababu watu kama hao ni kama hakuna kabisa. Hilo naweza kulisema kwa uhuru mkubwa,” amesema.
Amesema walipatana na Qares walipokuwa bungeni kwa sababu alijua kila anachosema ndicho alichokiamini. Kwa mujibu wa Jenerali, hilo lilimfanya kuwa mtu wa aina yake ikilinganishwa na wengine.
Amesema Qares alikuwa Mwenyekiti wa kundi la G55, lililotokana na wabunge wawili waliopeleka hoja bungeni ya kutengenezwa Serikali ya Tanganyika ndani ya mfumo wa Muungano, ili kuunga mkono hoja ya wabunge hao na kuipa nguvu.
“G55 ikaundwa ili kuunga mkono hoja hiyo kwa kuipa mashiko mapana zaidi na kuifanya isiwe ni hoja ya mbunge binafsi mmoja au wawili, lakini iwe ni hoja ya wabunge wengi kiasi kinachowezekana ili mtu asipate woga wa kuizungumzia,” amesema na kuongeza:
“Akachaguliwa Qares kuwa mwenyekiti kwa sababu ya kuangalia misimamo yake na jinsi alivyokuwa mtu mwenye misimamo inayoeleweka. Akaonekana yeye ndiye anaweza kuwa kiongozi na kweli, tulifanya kazi nzuri kwa kujibu hoja kwa hoja.”
Jenerali amesema unapofanya kazi kama hizo, utakumbana na ahadi za kukupotosha ili usiendelee na msimamo, lakini Qares alifanya kazi yake vizuri. Amesema alikuwa mtu aliyenyooka na kiasi cha unafiki kwake kilikuwa kidogo.
Mwanasiasa huyo mkongwe alikuwa kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), aliyewahi kutumikia nafasi mbalimbali, zikiwamo Mbunge wa Babati (1980 – 1995), Waziri wa Ushirika na Masoko (1989 – 1990), Waziri wa Utumishi (1996 – 2000) na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya (2000 – 2006).
Chifu Mwaihojo Mwambipile amesema anamkumbuka Qares akieleza walipofanya kazi pamoja Mwanza mwaka 1983, alionyesha ushirikiano, akijishusha kwa wananchi bila kujali wadhifa wake.
Amesema Qares alisimamia alichokiamini na alipenda kushirikiana na walio chini yake.
“Nikiwa Ofisa Mipango Miji Mwanza, yeye (Qares) alikuwa Ofisa Ushirika na Ujamaa. Baadaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya. Wakati nastaafu nilikuwa naye hapa Mbeya,” anasema na kuongeza:
“Kuna kipindi alikuwa anachinja mbuzi pale Nanenane. Hakuna namna naweza kumuelezea ila alijishusha bila kujali cheo chake. Hili ni pigo kubwa kwa Taifa.”
Mwandishi mkongwe mkoani Mbeya, Felix Mwakyembe, amesema Qares atakumbukwa kwa miradi ya maendeleo enzi za utawala wake mkoani humo, ikiwamo shule za mchepuo wa Kiingereza kama ya Mkapa.
Amesema katika kipindi cha uongozi wake, aliwapa nafasi na kushirikiana na wakurugenzi, akieleza misimamo yake katika kile alichoamini ili isogeze Mbeya kwenye maendeleo.
“Lile eneo la Shule ya Msingi Mkapa lilikuwa la soko la wafanyabiashara. Walisimika bendera ya CCM lakini aliwatimua, akaelekeza halmashauri kujenga shule hiyo, na yeye ndiye muasisi wa shule nne za mchepuo wa Kiingereza Mbeya.
“Aliruhusu wakulima kuuza mahindi kwa namna watakavyo, pale walipozuiwa kuuza mabichi, akiwaeleza waangalie ni wapi watapata faida. Uamuzi huo ulikuwa kinyume cha msimamo wa Serikali kwa wakati huo.”
Mkazi wa Kata ya Bagara, mjini Babati, Magdalena Ombay, amesema watamkumbuka Qares kwa msimamo wake thabiti kwani hakuwa na uoga katika kusimamia na kutetea jambo analoliamini.
Ombay amesema alikuwa akishiriki matukio ya kijamii akiwa nyumbani kwake, alikojishughulisha na kilimo.
Mkazi mwingine wa kijiji hicho, John Martin, amesema Qares hakuwa mtu wa kujikweza, alijitolea bila kubagua mtu yeyote.
Amesema jamii ya eneo hilo imepata pigo kwa kuondokewa na mtu makini, mahiri, mwenye msimamo usioyumba, na atakayekumbukwa kwa kuitumikia jamii.
Amesema licha ya Qares kuitumikia nchi kwenye nafasi za ubunge, uwaziri na ukuu wa mkoa, hakunyanyua mabega wala kujikweza kwa namna yoyote ile.