Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila amewataka Wakuu wa wilaya za Ilala,Temeke na Kigamboni, wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na wataalamu ndani ya Jiji hilo kuwa na ubunifu hususani kwenye kukabiliana na changamoto ya msongamano wa magari ili Jiji hilo liweze kuimarika kiuchumi na liendelee kuwa kivutio kwa wageni na watalii kutoka mataifa mbalimbali Duniani.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kilichokutanisha wakuu wa Wilaya za Ilala na Kigamboni,wakurugenzi wa halmashauri hizo,Katibu Tawala wa Mkoa huo pamoja na wataalamu kutoka TANROAD,TARURA na Mamlaka ya bandari TPA RC Chalamila amesema changamoto ya msongamano wa magari hususani malori inapaswa kutafutiwa suluhisho la kudumu ili kuepuka usumbufu ulioko kwa sasa.
Aidha RC Chalamila amewataka wakurugenzi wa Halmashauri kushirikiana na wataalam pamoja na watendaji wa mitaa na Kata kutumia njia rafiki kuelimisha wananchi hususani akinamama wanaouza chakula barabarani kujua umuhimu wa kutunza mazingira na kuacha kupika vyakula kandokando ya barabara.
Sanjari na hayo Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es salaam amezungumzia suala la uwepo wa hoteli za kitalii zitalazoweza kupokea viongozi kutoka nchi na mataifa mbalimbali ambapo amewataka wakurugenzi na wakuu wa wilaya kutazama namna ya kushirikiana na wamiliki majengo yaliopo katikati ya Jiji hususani jirani na Hayyat Regency hotel ili majengo yote hayo yajengwe hoteli za kitalii
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo akizungumza pia kwa niaba ya wakuu wa wilaya za kigamboni na Temeke amemuahidi Mkuu wa Mkoa huo kuwa wanakwenda kusimamia utekelezaji wa maelekezo hayo huku pia Katibu Mkuu wa chama cha wamiliki wa malori Tanzania TAMSTOA Issa John akisisitiza bandari kavu ya kwala iwe ndio suluhisho na ICD ziwe kilometa 30 kitoka mjini