Sababu za Serikali kupeleka maji Tabora kutoka Ziwa Victoria

Dodoma. Serikali imesema hadi kufikia Julai 2026, changamoto ya maji kwa Mkoa wa Tabora itakuwa historia baada ya mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika wilaya za Urambo, Sikonge na Kaliua kukamilika.

Mbali na hilo, pato la mtu mmoja mmoja katika mkoa huo limeongezeka kutoka Sh1.77 milioni mwaka 2020 hadi Sh1.85 milioni mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 4.5.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa, Julai 11, 2025, na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, wakati akielezea mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita ya mkoa wake katika ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo), jijini Dodoma.

Chacha amesema maji ya Ziwa Victoria kwa sasa yanatumika katika Wilaya ya Nzega, Igunga, Uyui na Tabora Mjini, na kuwa sehemu iliyobakia ni wilaya za Urambo, Sikonge na Kaliua.

Amesema wilaya hizo zitapelekewa maji hayo kupitia awamu ya pili ambayo utekelezaji wake umefikia asilimia 75, na kuwa hadi kukamilika unatarajiwa kutumia Sh143 bilioni.

“Mradi ukikamilika, kutabakia adha ndogondogo ya connection (maunganisho) nyumba kwa nyumba, lakini adha kubwa iliyokuwa ikiwakumba wananchi wa maeneo hayo haitakuwepo,” amesema.

Amesema sababu ya Serikali kuwekeza nguvu kubwa katika kutoa maji Ziwa Victoria ni kutopatikana maji baada ya uchimbaji wa visima, kutokana na kiwango cha juu cha maji chini ya ardhi (water table) kutokuwa sawa.

“Tumeingia migogoro mingi na wakandarasi, lakini kiuhalisia maji chini hayapo, ndiyo maana Serikali imeamua kuachana na uchimbaji wa visima virefu – tunaleta maji ya Ziwa Victoria,” amesema.

Chacha amesema wamebakiza asilimia 15 kufikisha maji katika wilaya zote za Mkoa wa Tabora, na adha ya maji itakuwa historia kufikia Julai 2026.

Amefafanua kuwa katika Sikonge, mradi huo utakamilika mwishoni mwa 2025, na sehemu kidogo ya Urambo na Kaliua itakamilika Julai 2026.

Kuhusu hali ya uchumi, Chacha amesema hali ya uchumi ya mkoa huo imeendelea kuimarika, ambapo pato halisi la mkoa limekua kutoka Sh5.4 trilioni mwaka 2020 hadi Sh6.3 trilioni mwaka 2024, sawa na ukuaji wa asilimia 17.

“Vilevile, pato la mtu mmoja mmoja limeongezeka kutoka Sh1.77 milioni mwaka 2020 hadi Sh1.85 milioni mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 4.5,” amesema.

Kwa upande wa viwanda, Chacha amesema katika kipindi hicho cha miaka minne, kumeanzishwa viwanda vikubwa vitatu, vya kati 19, vidogo 984 na vidogo sana 324.

Amesema miongoni mwao ni kiwanda cha Serikali cha kutengeneza nguzo za umeme za zege, ambacho ujenzi wake uko katika hatua za mwisho.

Pia amesema kiwanda kikubwa cha uchakataji wa zao la tumbaku kinajengwa katika mkoa huo, kutokana na mkoa huo kuzalisha asilimia 70 ya tumbaku inayozalishwa nchini, ambayo ni kilo milioni 114.

Aidha, mkuu huyo wa mkoa amesema katika kipindi cha kati ya Machi 2021 hadi Juni 2025, mkoa huo umetekeleza miradi mikubwa yenye thamani ya Sh15 trilioni.

“Miradi imetekelezwa kwa mafanikio makubwa katika sekta zote, zikiwemo afya, elimu, miundombinu ya usafiri na usafirishaji, maji, nishati, kilimo, mifugo, viwanda, biashara,uwezeshaji wananchi kiuchumi,” amesema.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Zamaradi Kawawa, amesema mkutano huo ni sehemu ya mfululizo wa mikutano ya wakuu wa mikoa kuelezea mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita.

“Mkoa huu lazima tuuheshimu kwa kuwa ndio kinara nchini kwa uzalishaji wa tumbaku, na unaingiza fedha nyingi za kigeni ambazo zinatumika kwa maendeleo ya wakulima na nchi kwa ujumla wake,” amesema

Related Posts