Dodoma. Serikali imetaja njia mbadala ya kumaliza ama kupunguza rushwa, ni kujenga mifumo ambayo itakuwa wazi katika utoaji wa huduma za kiserikali ikiwemo kutokutana moja kwa moja na wenye kutoa uamuzi huo, huku ikieleza ni muhimu rushwa kutamka wa kwa uwazi kuelekea uchaguzi mkuu.
Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Julai 11, 2025 wakati wakati akifungua kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Mapambano ya rushwa Afrika yanayofanyika Jijini Dodoma.
Wakati Simbachawene akitoa kauli hiyo, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Profesa Palamagamba Kabudi amesema mwaka huu wa uchaguzi ni lazima suala la rushwa lizungumzwe kwa nguvu zote kwani linaweza kuharibu taswira nzima ya nchi.
Simbachawene amesema kuwa huduma za Serikali hazipaswi kutoa nafasi ya watu wenye kufanya maamuzi kukutana moja kwa moja na watu wenye mahitaji ya huduma hivyo teknolojia inapaswa kuchukua nafasi yake katika hilo.
Waziri Simbachawene amesema licha ya tatizo la Rushwa nchini, lakini Tanzania imeendelea kufanya vizuri kwenye mapambano yake kulingana na taarifa za vyombo vya kimataifa.
“Tanzania ilianza kuadhimisha siku ya kupinga rushwa tangu mwaka 2018, tumeendelea kufanya vizuri kwenye mapambano dhidi ya rushwa na hasa kwenye hii kaulimbiu ya mwaka huu ya “Kuza Heshima ya Binadamu kwenye Mapambano dhidi ya Rushwa, kikubwa tuongeze mbiu,” amesema Simbachawene.
Akitoa mada kwenye kwa washiriki wa kongamano hilo, Profesa Palamagamba Kabudi amesema falsafa za Rais Samia zimepelekea kuwa na chachu ya kulinda utu, kuleta mabadiliko na kujenga misingi imara katika jamii ya Tanzania.
Profesa Kabudi amebainisha kuwa falsafa hiyo imekuwa ni nguzo muhimu katika kujenga jamii yenye uzalendo huku akieleza kuwa, mtu anayekula rushwa ni siyo mwema katika jamii.
Amesema katika kuelekea uchaguzi mkuu nchini, ni muhimu kuishi katika falsafa hiyo ili kuwa sehemu ya historia ya Tanzania kwa kuwa ndani yake ipo siri kubwa ya utaifa na uzalendo wa kweli.
Ametoa wito kwa viongozi, vijana na jamii kwa ujumla kuwa hakuna njia ya mkato kwenye mafanikio hivyo wahakikishe wanavuja jasho ili kupata kilicho cha haki.
Amesema rushwa ina tabia ya ujauzito, huanza kidogo kidogo haionekani na baadaye inakuwa kubwa na kuonekana kwa hivyo ikionekana ndiyo utu wa wa mtu unapoanza kuondoka na kuondoa utu wa watu wengine.
Mjumbe wa Bodi ya Umoja wa Afrika ya Ushauri juu ya Rushwa Joseph Maope, amesema mapambano dhidi ya rushwa yatawezekana kwa jamii kushikana na kushauriana juu ya madhara.
Maope amesema katika Umoja wa Afrika Tanzania inatajwa kuwa miongoni mwa nchi zinazosifika kwenye mapambano hayo licha ya ukweli kuwa tatizo bado lipo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Crispin Chalamila amesema mapambano dhidi ya rushwa yanapaswa kupiganwa na kila mtu kwani huweza kupotosha haki na kurudisha maendeleo ya watu.