Dar es Salaam. Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Francis Ndulane, amepata ajali na kuvunjika mguu wakati akiwa kwenye mchakato wa mchujo wa watiania wa ubunge kwenye jimbo hilo ndani ya chama.
Kuumia kwa mbunge huyo kumethibitishwa leo Ijumaa, Julai 11, 2025, na Meneja Uhusiano wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Patrick Mvungi, alipozungumza na Mwananchi Digital.
Mvungi amesema kuwa Ndulane alipokelewa katika taasisi hiyo siku tano zilizopita na ameanza kupatiwa matibabu.
“Ni kweli tumempokea mbunge huyo wa Kilwa na anaendelea kupata matibabu hadi leo akiwa chini ya uangalizi wa madaktari na hali yake kwa sasa inaendelea vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji,” amesema meneja huyo.
Akizungumza na Mwananchi leo kwa njia ya simu akiwa hospitalini, mbunge huyo amesema alitumbukia kwenye shimo la gereji lililopo kwenye karakana ya Chuo cha Maendeleo cha Kilwa Masoko, ambako kulikuwa kunaendeshwa usaili wa watiania wa ubunge na madiwani.
“Ilikuwa saa sita hivi nilikuwa naongea na simu, basi nikajikuta napitiliza na kutumbukia kwenye shimo ambalo sikuliona, nikawa nimeumiza mshipa wa paja, ukawa umevunjika,” amesema Ndulane.
Mbunge huyo amesema shimo hilo ni yale marefu ambayo gari inakuja halafu mafundi wanatengeneza kule chini, ambalo lina urefu wa kama mita mbili hivi.
Akizungumzia hali yake kwa sasa, amesema:”Hali yangu inaendelea vizuri, namshukuru Mungu kwa kweli nimepata huduma nzuri na ninaendelea vizuri.
“Tangu nilipofikishwa hapa tarehe sita usiku, tarehe saba nikafanyiwa operesheni, kuanzia tarehe nane nikaanza kufanyishwa mazoezi kidogo na tarehe tisa nikaendelea kufanyiwa mazoezi na kupata tiba nikiwa chini ya uchunguzi wa madaktari.
“Ni imani yangu ndani ya siku mbili, tatu pengine Mwenyezi Mungu akipenda nitaruhusiwa,” amesema Ndulane.
Katibu Mwenezi wa CCM, Mkoa wa Lindi, Patrick Magarinja, amesema Ndulane alipata ajali hiyo akiwa katika Chuo cha Maendeleo Kilwa Masoko, ambapo usaili wa mchujo wa watiania wa madiwani na wabunge ulikuwa ukifanyika hapo.
Magarinja amesema mbunge huyo akiwa hapo kusubiri afikiwe zamu yake, alikuwa anaongea na simu, lakini kwa bahati mbaya mbele yake kulikuwa na shimo ambalo hakuliona, jambo lililomfanya adumbukie na kuvunjika mguu.
“Katika ajali hiyo, Ndulane aliumia pakubwa, jambo lililomfanya akimbizwe hospitalini na baadaye kuhamishiwa kwenye Taasisi ya Mifupa MOI kwa ajili ya matibabu zaidi,” amesema katibu mwenezi huyo.
Mmoja wa mashuhuda aliyekuwepo wakati mbunge huyo anapata ajali hiyo, ambaye hakutaka jina lake liandikwe, amesema ilikuwa saa nne asubuhi kuelekea saa tano, walimuona akiwa anaongea na simu huku anatembea bila kujua kuwa alipokuwa anaelekea kulikuwa na shimo.
Wakati akiwa anafanya hivyo, chanzo hicho kimesema watu walikuwa wakimpigia kelele kuwa huko anakoelekea kuna shimo, lakini ni kama hakuwa anawasikia na mwisho akadumbukia na kupata majeraha hayo.
“Yaani ile ajali ya mbunge nimeishuhudia live, alipokuwa anaongea na simu na kuelekea lilipo shimo, tulijitahidi kumpigia kelele na watu tuliokuwepo pale kuwa asiendelee kwenda, lakini ndio hivyo hakuwa anasikia.
“Nadhani alikuwa busy na maongezi ya kwenye simu na hivyo kutoweza kutusikia. Kiukweli ameumia vibaya kwani hadi mfupa wa mguu ulikuwa umetoka nje,” kilieleza chanzo hicho.
Katika hatua nyingine, Mwalimu Mustapha Rumeze, ambaye alikuwa akitarajia kwenda kuchukua fomu ya kutoa kuteuliwa kuwania ubunge katika jimbo hilo, amefariki dunia katika ajali ya gari akiwa njiani kuelekea Kilwa.
Taarifa za ajali iliyomhusisha kada wa CCM, Rumeze, zimethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Protas Mutayoba.
Kamanda Mutayoba amesema ajali hiyo ilitokea baada ya gari aina ya Toyota Land Cruiser, ambalo kada huyo alikuwa akisafiria pamoja na watu wengine, kupasuka tairi la nyuma kisha kupoteza mwelekeo na kutoka nje ya barabara.
“Ni kweli ajali hiyo ilitokea wiki mbili zilizopita eneo la Kibiti, na marehemu alikuwa kwenye gari na watu wengine ambao walipata majeraha.
“Hata hivyo, yeye alipoteza maisha wakati akiwa katika Hospitali ya Mchukwi alipopelekwa kupatiwa matibabu,” amesema kamanda huyo.
Chanzo cha karibu kutoka ndani ya CCM Kilwa kilisema ajali hiyo aliipata usiku wa kuamkia Juni 29 akiwa maeneo ya Kibiti, akiwa na gari yake ndogo kuelekea Kilwa kuchukua fomu.
“Ni kweli Rumeze alifariki ikiwa ni siku mbili kabla ya kutaka kwenda kutangaza nia. Kifo hicho kimetuumiza kama wana CCM na vijana wenzake,” kimesema chanzo hicho.