Simba imefikia makubaliano ya kumsajili kiungo wa CS Sfaxien, Balla Moussa Conte leo Ijumaa, Julai 11, 2025.
Kiungo huyo wa ulinzi raia wa Guinea mwenye umri wa miaka 21, alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja na Sfaxien unaofikia tamati 2026 ambao Simba imeuvunja na kumnasa mchezaji huyo.
Conte amekuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo wa Sfaxien ambapo amekuwa chaguo la kwanza la timu hiyo ya Tunisia ambayo iliishia katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika 2024/2025.
Katika msimu uliomalizika Conte amecheza mechi 23 za Ligi Kuu ya Tunisia akiwa na kikosi cha Sfaxien huku akionyeshwa kadi saba za njano.
Amecheza mechi sita za Kombe la Shirikisho Afrika huku pia akicheza mechi mbili za Kombe la Klabu Bingwa kwa Nchi za Kiarabu.
Kiujumla, Conte amecheza idadi ya mechi 34 za Ligi Kuu ya Tunisia akiwa na kikosi cha Sfaxien.
Usajili wa Conte ni mwanzo wa Simba kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao baada ya kuwapa mkono wa kwaheri baadhi ya wachezaji wake.
Katika nafasi ya kiungo ambayo Conte anaicheza, Simba imeshaachana na Fabrice Ngoma na Augustine Okejepha.