TABORA KUJENGA KIWANDA CHA TUMBAKU

:::::

Na Ester Maile Dodoma 

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paulo Matiko Chacha, amesema kuwa kuimarika kwa upatikanaji wa mbolea mkoani humo kumechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa uzalishaji wa zao la tumbaku kutoka kilo 29,829,742 mwaka 2021 hadi kilo 62,964,460 mwaka 2025.

Akizungumza leo Ijumaa Julai 11, 2025 katika Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) jijini Dodoma, wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mhe. Chacha amesema hali ya upatikanaji wa mbolea imeimarika kutoka tani 34,109 mwaka 2020/2021 hadi tani 61,504 mwaka 2024/2025.

“Kuongezeka kwa upatikanaji wa pembejeo, hasa mbolea, kumechochea ukuaji wa uzalishaji wa tumbaku. Matokeo yake, wakulima wa tumbaku Tabora wanatarajiwa kupata kati ya Shilingi Bilioni 741 hadi 750 kutokana na mauzo ya zao hilo,” amesema Chacha.

Aidha, amebainisha kuwa bei ya tumbaku imepanda kutoka wastani wa dola 1.0 kwa kilo hadi dola 2.0 hadi 2.7 kwa kilo kwa sasa, hali inayoongeza mapato ya wakulima na uchumi wa mkoa kwa ujumla.

Katika sekta ya madini, Chacha amesema Serikali imeendelea kufanya maboresho makubwa, ambapo uzalishaji wa madini umeongezeka kutoka tani 0.34 mwaka 2020 hadi tani 0.8 mwaka 2025.

“Tumeongeza pia mapato ya fedha za kigeni kupitia uuzaji wa madini kutoka Dola za Marekani milioni 15.07 mwaka 2020 hadi Dola milioni 50.69 mwaka 2025,” amesema.

Vilevile, masoko ya madini yameongezeka kutoka soko moja na kituo kimoja kidogo mwaka 2020 hadi soko moja na vituo vitano mwaka 2025. Idadi ya leseni kwa wachimbaji wadogo pia imeongezeka kutoka 136 mwaka 2020 hadi 574 mwaka 2025.



 

Related Posts