Ukweli lishe kwa wagonjwa wenye kisukari

Dar es Salaam. Katika jamii nyingi, suala la lishe kwa mtu mwenye kisukari limezungukwa na taarifa nyingi zinazochanganya.

Wengi huamini kuwa mtu mwenye kisukari haruhusiwi kula vyakula fulani kabisa.

Wengine hufikiri lazima ale chakula maalum kinachopatikana kwa gharama kubwa, huku baadhi wanamini mtu mwenye kisukari hawezi tena kufurahia mlo wa kawaida kama wengine.

Ukweli wa kisayansi na kimaisha ni tofauti kabisa na dhana hizi potofu, ambazo zikiendelea kushamiri, huongeza hofu, unyanyapaa na hata kuchangia utapiamlo miongoni mwa watu wanaoishi na kisukari.

Ni muhimu kuelewa kwamba lishe sahihi ni msingi wa udhibiti wa kisukari. Hata hivyo, lishe hii si ya kifahari kama wengi wanavyoamini. 

Kanuni kuu ni kula chakula chenye uwiano sahihi na virutubisho, wanga, protini, mafuta, vitamini, madini na maji ya kutosha. Kinachobadilika kwa mtu mwenye kisukari ni umakini wa ulaji wa wanga na muda wa kula. 

Wengi wanaamini kuwa mtu mwenye kisukari hatakiwi kula wanga kabisa. Watu wengi hudhani wanga kama wali, ugali, viazi au mihogo ni marufuku. Ukweli ni kwamba mwili unahitaji wanga kwa ajili ya nishati. Kile kinachoshauriwa ni kuchagua wanga wenye nyuzinyuzi nyingi kama vile ugali wa dona, viazi,maboga, mihogo au viazi vitamu kwa kiasi kinachodhibitiwa.

Jamii nyingi huamini kuwa mtu mwenye kisukari akila matunda, anajihatarisha zaidi. Hili pia si sahihi. 

Matunda ni sehemu muhimu ya lishe bora, lakini ni lazima kuchagua matunda yenye sukari ya wastani kama papai, chungwa, embe, tufaa  na matunda mengine ila ulaji wake pia uwe ni wa kiasi sahihi.

Wengine wanamini kuwa mtu mwenye kisukari haruhusiwi tena kula chakula chochote kwenye sherehe na kushiriki hafla.

Hili husababisha unyanyapaa na kuwafanya wengine kuwaona wagonjwa wa kisukari kama watu wasioweza kufurahia maisha. 

Ukweli ni kwamba mtu mwenye kisukari anaweza kula chakula chochote, ila anapaswa kufanya uamuzi ambao hautaweza kupandisha viwango vya sukari.

Changamoto inayochangia upotoshaji huu ni ukosefu wa elimu sahihi kuhusu kisukari. Watu wengi wanategemea taarifa kutoka kwa marafiki, mitandao ya kijamii au kusikia habari za mtaani badala ya kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa lishe na madaktari.

Kisukari si hukumu ya kuishi maisha ya kula kwa mashaka au kuachana na vyakula vyote vizuri. Badala yake, ni muhimu kwa wenye kisukari kuanza kujifunza, kupanga na kufurahia mlo wa afya wenye uwiano sahihi. 

Kushiriki kwenye mafunzo ya lishe bora, na chakula cha pamoja kama familia,ni kati ya mambo ya kudumishwa na mgonjwa.

Kisukari hakitakiwi kuwa sababu ya kuvunjika moyo, bali sehemu ya maisha inayodhibitika na hatimaye mgonjwa  kuishi kwa matumaini.

Related Posts