BAADA ya kuanza vibaya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON), timu ya taifa ya soka ya wanawake, Twiga Stars usiku wa leo inarudi tena uwanjani kutesti zali kwa kukabiliana na watetezi wa taji hilo, Afrika Kusini ‘Banyana Banyana’.
Twiga ilianza kwa kulambwa bao 1-0 na Mali katika mechi ya kwanza ya Kundi C, iliyopigwa Jumatatu iliyopita na leo Ijumaa inashuka Uwanja wa d’Honneur d’Oujdakuanzia saa 4:00 usiku kusahihisha makosa mbele ya watetezi walioanza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ghana.
Timu hiyo ya Tanzania inahitaji ushindi mbele ya Banyana Banyana ili kuweka hai matumaini ya kuvuka makundi kwenda hatua ijayo kwani kipigo chochote kitaiweka bayana kwani tayari watetezi wana pointi tatu sawa na Mali ambayo mapema saa 1:00 usiku itavaana na Ghana inayoburuza mkia.
Hata hivyo, mechi hiyo si rahisi kwa Stars kutokana na rekodi ya Afrika Kusini, iliyocheza Kombe la Dunia mara mbili na mara ya mwisho ilikuwa ni 2023 ilipoishia 16 Bora.
Mechi iliyopita, Stars ilicheza vizuri kwa kumiliki mpira lakini hakukuwa na maelewano mazuri katika safu ya ushambuliaji, ambayo iliongozwa na Stumai Abdallah aliyepoteza mipira mingi.
Ujio wa Opah Clement, aliyekosekana mchezo uliopita kutokana na kadi nyingi za njano, utaongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji ambalo lilikosa utulivu kwani ni mshambuliaji mwenye nguvu na maamuzi langoni mwa wapinzani.
Licha ya ubora wa timu hiyo, lakini ina madhaifu kwenye baadhi ya maeneo na hayo yanaweza kuwa faida kwa Stars.
Banyana Banyana hupenda kushambulia kwa idadi kubwa ya wachezaji, hasa kupitia mawinga, hivyo huacha nafasi kubwa nyuma kupitia mabeki wa pembeni. Hivyo kama Stars itashambulia kwa kushtukiza mara kwa mara, itawachanganya wapinzani.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Kocha wa Stars, Bakari Shime alisema wanafahamu ugumu wa mchezo huo, hivyo wamejiandaa kuhakikisha makosa waliyofanya mchezo uliopita hayajirudii.
“Tulitengeneza nafasi nyingi mechi iliyopita, tulikuwa na nafasi nzuri ya kufunga mabao lakini hayo tumeyaacha na tumeelekezana kuelekea mechi na Afrika Kusini. Tunaamini tutafanya vizuri.”