WAJASIRIAMALI WANUFAIKA WA CAMFED WAONYESHA BIDHAA SABASABA

 

Mmoja wa wajasiriamali wanufaika wa Shirika la CAMFED Tanzania akizungumza kwenye Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara – maarufu kama Sabasaba wanayoshiriki kutangaza biashara wanazozifanya kwa sasa.



Sehemu ya wajasiriamali wanufaika wa Shirika la CAMFED Tanzania wakiwa na bidhaa zao mbalimbali kwenye Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara – maarufu kama Sabasaba wanayoshiriki kutangaza zaidi biashara hizo.

BAADHI ya mabinti waliofanikiwa kunufaika na programu za Shirika la CAMFED Tanzania wamejitokeza na kushiriki kwenye kwenye Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara – maarufu kama Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam huku wakivutiwa na hatua hiyo waliofikia.

Wakizungumza kwenye maonesho hayo, Winfrida Kihali kutoka Wilaya ya Ulanga, mkoani Morogoro, amesema kuwa Shirika la CAMFED limechangia kwa kiwango kikubwa kwenye mafanikio ya maisha yake, kwani limesaidia kumpa ujuzi wa ujasiriamali, ambapo kwa sasa amefika Sabasaba kuonesha bidhaa zake kwa kujiamini zaidi.

Bi. Kihali amesema CAMFED, imekuwa ikitoa mikopo isiyo na riba, kuanzia shilingi 300,000 hadi 500,000 ambazo ndio ziliomuwezesha hadi leo kuwa mjasiriamali anayejitegemea. Ameongeza kuwa baadhi ya wanufaika waliopo chini ya ‘Guide rules’ hupokea kiasi cha shilingi 270,000, huku wengine ambao si wanachama wa CAMFED wakipokea kiasi cha shilingi 200,000 kuanzisha biashara ndogondogo.

Aidha amebainisha kuwa shirika hilo limewaunganisha wanufaika wake na Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC), jambo ambalo limefanikisha kushiriki Maonesho ya 49 ya biashara Sabasaba, ambapo wameendelea kupata ujuzi mbalimbali ikiwemo namna ya kuwasiliana na wateja, kufunga vifurushi vya bidhaa zao kisasa pamoja na kuboresha chapa za bidhaa wanazozalisha.

“Msichana akielimika, jamii nzima imeelimika. Wasichana wakielimishwa wanakuwa na uelevu wa kufanya mambo makubwa. Mimi mwenyewe nilisaidiwa na CAMFED nikiwa kidato cha tatu, na baadaye nikapelekwa chuo kusomea Maendeleo ya Jamii,” alisema Bi. Winfrida Kihali.

Kwa upande wake, mnufaika mwingine Bi. Faudhiati Simba kutoka Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, ameeleza kuwa alisaidiwa na CAMFED wakati wazazi wake waliposhindwa kumhudumia mahitaji muhimu ya shule.

“Kama siyo CAMFED, nisingeweza kufikia ndoto zangu. Walinisaidia kuendelea na elimu ya sekondari na kisha kunisaidia kujiunga na chuo kwa kushirikiana na Bodi ya Mikopo,” alisema.

Aidha Faudhiati alisema hata akiwa chuoni, CAMFED hawakumuacha, walimsaidia kujiunga na programu mbalimbali za kujifunza kuhusu biashara. Kupitia mafunzo hayo, alianza biashara ya kuoka keki kwa kutumia jiko la mkaa, na sasa anamiliki ‘bakery’ inayouza vitafunwa mbalimbali.

Pamoja na hayo, mnufaika huyu anaiomba Serikali kusaidia mashirika kama CAMFED ambayo yanasaidia wasichana, vijana na wanawake kufikia ndoto zao za kielimu na kimaisha ili yaweze kuinua vijana wengi zaidi na kuchangia kuinua uchumi wa taifa.

“Shirika kama CAMFED linahakikisha mtoto wa kike anafikia malengo yake kielimu na kibiashara. Serikali iendelee kushirikiana na mashirika haya ili kuwasaidia wasichana wengi waliopoteza mwelekeo,” alisema Bi. Simba.

Naye Bi. Jamila Masesa kutoka mkoani Tabora ametoa wito kwa jamii, wazazi na walezi kuwa wabunifu katika malezi ya watoto wa kike, kwa kuwa wao hukumbana na changamoto nyingi. Amehimiza jamii kuamini kuwa mtoto wa kike akipewa nafasi na kuwezeshwa, anaweza kufikia ndoto zake.

“Wazazi na walezi wanapaswa kuwa walinzi wa ndoto za watoto wa kike kwa kuwapa nafasi, kuwahamasisha na kuwaamini. Kupitia afua mbalimbali, wawezeshwe kielimu, kiuchumi, kijamii na hata katika uongozi,” alisema Bi. Jamila.

Related Posts