Wajutia wakiahidi kuwa walinzi baada ya kutiwa mbaroni, kutozwa faini kisa uvuvi haramu

Unguja. Baada ya kukamatwa na kutozwa faini kwa kosa la kuendesha uvuvi haramu, wavuvi zaidi ya 40 wamesema wamepata funzo na kuahidi kuwa mabalozi wa kutokomeza uvuvi huo.

Wavuvi hao walikamatwa na Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM) wakiwa na boti moja ya kisasa na mitumbwi minane katika ghuba ya Chwaka ambalo pamoja na kuendesha uvuvi haramu lakini pia walikutwa katika eneo la uhifadhi ambalo haliruhusiwi kuingia bila vibali maalumu.

Wakizungumza wakati wa kurejeshewa zana zao za uvuvi Julai 12, 2025 baada ya kula mvuvi kulipa faini ya Sh100,000 wavuvi hao wamesema hawatarudia kufanya kosa hilo na wanakwenda kuwa mabalozi kwa wengine kuachana na uvuvi huo.
“Ni kweli tulifanya makosa, lakini sasa tumeelimika na tunashukuru kwa elimu tuliyopata, nasi tutaifikisha kwa wavuvi wenzetu ili kwa pamoja tufanye kazi kwa kuzingatia sheria na ustawi wa bahari na rasilimali zilizomo,” amesema mmoja wa wavuvi hao Khamis Hassan Khamis
Mvuvi mwingine kutoka shehia ya Chwaka, Haroub Haji Hussein amesema amesema wamekuwa wakifanya hivyo mara kwa mara licha ya kufahamu kuwa ni kosa lakini ilikuwa ni tamaa lakini kwa sasa wamejifunza kuheshimu sheria.
“Sio kweli kwamba tunafanya kitu hiki hatujui ila ni kwasababu ya tamaa maana eneo la hifadhi samaki wanakuwa wengi, lakini tumejifunza na tunaahidi hatutafanya hivi tena sisi wenyewe tutakuwa walinzi kwa watakaotaka kuharibu,” amesema.
Amezishukuru taasisi husika kuwapa elimu ya matumizi sahihi ya zana za uvuvi na kuheshimu misingi na sheria inayowekwa katika kulinda na kutumia vyema rasilimali za baharini kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.

Awali Mkuu wa kambi ya KMKM Marumbi Wilaya ya Kati, Luteni Hussein Kasssim Makame amesema ulinzi zaidi na madhubuti unahitajika katika ghuba ya Chwaka kutokana na kukithiri kwa uvuvi haramu unaofanywa na baadhi ya wavuvi, kitendo kinachokiuka utaratibu uliowekwa na serikali.

Amesisitiza kuwa kikosi chake kitaendelea kuimarisha doria za mara kwa mara katika ghuba hiyo kuhakikisha uvuvi haramu unakoma.

Amesema wavuvi hao walikamatwa na kikosi hicho takribani miezi mitatu iliyopita vikihusishwa na uvuvi haramu katika maeneo ya ghuba ya Chwaka.

Luteni Makame amesema sheria zilizowekwa na serikali hazilengi kuwakomoa wananchi, bali zimezingatia ustawi wa mazao ya baharini kwa faida ya sasa na baadaye.

Amesema uvuvi haramu una athari kubwa kwani unachangia uharibifu wa matumbawe yanayotegemewa kwa uzazi na ukuaji wa samaki, hivyo ukidhibitiwa wavuvi watapata tija na pia taifa kunufaika.

“Kuna matukio mengi mabaya yanayotokea baharini ikiwemo uharamia na magendo, lakini makosa mengi tunayokamata ni haya ya uvuvi haramu. Tunajitahidi sana kupambana na hali hii na haya ndio matokeo yake,” amesema Makame.

Ameshauri kuongezwa vyombo na vifaa vingine vya kiulinzi, ili kikosi hicho kiweze kufanya doria nyingi kwa uhakika, kupunguza na hatimaye kukomesha kabisa uvuvi haramu na uharamia mwingine unaofanyika baharini.
 

 Ofisa Uvuvi Wilaya ya Kati, Ali Mwalimu Mahfoudh kutoka Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, aliwasisitiza wavuvi kufuata sheria za uvuvi zinazolenga kuyatunza maeneo ya hifadhi ya bahari kwa maslahi mapana ya taifa sasa na baadaye.

“Kupitia ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Wilaya, Idara ya uvuvi imekuwa ikifuatilia kwa karibu nyendo za wavuvi ili kuhakikisha wanafuata sheria na bahari yetu na mazao yake inakuwa salama,” amesema

Amesema kuzuia vyombo vya wavuvi kwa muda mrefu si jambo jema kwani linaathiri kipato chao kinachotegemewa kuendesha familia kwa mahitaji mbalimbali ya msingi na hata mashine kuharibika na kusababisha hasara.

Amewataka wabadilike na kuacha kuvua kimazoea ili azma ya serikali kukuza uchumi wa buluu ilete ufanisi kwa wote, akisema kufuata sheria kunamuweka mtu huru na kuepukana na hofu ya kukamatwa na kuingia hatiani.

“Ili kuepuka hasara zote hizi ni vyema tukafuata sheria na kujiepusha na uvuvi haramu, maana pamoja na hasara sheria haitasita kuchukua mkondo wake, kisha zinatozwa faini huku mkishindwa kufanya kazi,” amesema

Hivi karibuni Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi ilisema kwamba kutokana na doria zinazoendelea kufanywa na uhifadhi wa bahari kumeongeza tija ya uzalishaji wa samaki kutoka tani zaidi ya 38,000 mwaka 2020 hadi zaidi ya tani 88,000 mwaka 2024 sawa na asilimia 107.

Kwa kipindi hicho zaidi ya doria 1500 zimefanywa na kuzaa matunda hayo.

Related Posts