ALIYEKUWA beki wa kushoto wa KMC, Rahim Shomary ameziingiza vitani timu mbili za National Bank of Egypt SC na Haras El Hodood zote za Misri zilizoonyesha kuvutiwa na uwezo mkubwa wa nyota huyo, kwa ajili ya kuzichezea msimu ujao.
Nyota huyo amemaliza mkataba na KMC na hakuna mazungumzo mapya yaliyofanyika ili kuongeza mwingine na wawakilishi wake walikuwa Misri kwa ajili ya kumtafutia timu, baada ya dili lake la kwenda Al-Hilal Omdurman ya Sudan kuota mbawa.
Awali nyota huyo alikuwa akihitajika na Al-Hilal iliyoonyesha nia ya kumhitaji mapema, ingawa dili hilo limekufa rasmi, baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Florent Ibenge aliyemhitaji kuondoka kikosini na kujiunga na Azam FC.
Baada ya dili hilo kushindikana, ndipo wawakilishi wa mchezaji huyo wakafanya mazungumzo na National Bank of Egypt SC na Haras El Hodood ambazo zilihitaji kwanza kumfanyia majaribio ili kuona uwezo wake kabla ya kufanya uamuzi.
“Wamevutiwa na uwezo wake na baada ya kufanya majaribio katika timu zote mbili, kilichobakia ni mazungumzo kuhusu masilahi binafsi, kama tutafikia mwafaka mzuri basi atasaini mojawapo kati ya hizo,” alisema msimamizi wa mchezaji huyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula alisema Rahim ni miongoni mwa nyota wa kwanza wa timu hiyo kupewa mkono wa kwaheri, baada ya kushindwa kufikia makubaliano ya kusaini mkataba mpya aliowekewa mezani.