MKUU wa Mkoa Tabora Mhe Paulo Chacha amesema kuwa katika moja ya mafanikio ya Mkoa huo ni pamoja Watalii wa Ndani kuongeza kutoka Watalii 1,283 mwaka 2020 hadi kufikia Watalii 7,397 mwaka 2025 hii ni mara baada ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuzindua filamu ya Royal Tour ambayo imewezesha Sekta hiyo ya Utalii kupokea Watalii wengi kila mwaka na kupelekea kuongezeka kwa mapato katika Sekta hiyo.
RC Chacha ameyaeleza hayo mapema Leo hii Jijini Dodoma Julai 11,2025 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari akielezea mafanikio ya Mkoa wake katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita.
Ambapo pia amesema misitu ya hifadhi imeongezeka kutoka misitu 6 mwaka 2020 hadi misitu 37 mwaka 2025 sambamba na upandaji wa miti takriban 1,500,000 ikiwa ni sawa na asilimia 80 ya lengo la Serikali.
“Mara baada ya kuingia madarakani Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua filamu ya Royal Tour, Filamu hiyo imewezesha sekta ya Utalii kuanza kupokea watalii wengi kila mwaka na hivyo kuongeza mapato katika sekta hiyo,ambapo Mkoa wa Tabora umepata mafanikio makubwa katika sekta hii ambayo ni pamoja na Idadi ya watalii wa ndani waliotembelea Mkoa imeongezeka kutoka watalii 1,283 mwaka 2020 hadi 7,397 mwaka 2025;Mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka shilingi 6,167,860 mwaka 2020 hadi shilingi 26,622,674 mwaka 2025”.
” Viwanda 04 vya kuchakata na kufungasha Asali vimejengwa;Uzalishaji wa Asali umeongezeka kutoka tani 1,868.6 mwaka 2020 hadi tani 2,002.48 kwa mwaka 2025″.
“Misitu ya hifadhi ya vijiji imeongezeka kutoka misitu 6 yenye ukubwa wa ekari 11,952.5 mwaka 2020 hadi misitu 37 yenye ukubwa wa ekari 330,780.75 mwaka 2025 na Miti takriban 1,500,000 imepandwa ambayo ni asilimia 80 ya lengo la Serikali kwa mwaka”.
Aidha Mkuu wa Mkoa huyo amesema kuwa mwaka 2020 Mkoa ulikuwa na Mahakama za mwanzo 41lakini hadi kufikia 2025 Mkoa una Mahakama za mwanzo 43, ambapo pia Mkoa ulikuwa Mahakama za Wilaya 6 hadi kufikia Aprili, 2025 Mkoa una Mahakama 7, pamoja na kuwepo kwa vitendo vya rushwa 191 mwaka 2020 lakini kutokana jitihada mbalimbali zilizofanyika vitendo vya rushwa vimepungua hadi 179 mwaka 2025.
Mkoa wa Tabora una ukubwa wa kilometa za mraba 75,685. Kilometa za mraba 75,173 ni eneo la nchi kavu, kati yake kilometa za mraba 20,199 sawa na asilimia 26.6 zinafaa kwa kilimo; kilometa za mraba 34,501 sawa na asilimia 45.6 ni eneo la misitu ya hifadhi na Kilometa za mraba 20,473 sawa na asilimia 27.1 ni eneo la makazi. Eneo la maji ni Kilometa za mraba 512 sawa na asilimia 0.7.