Watatu Simba wajiandaa kutua Yanga

SIMBA Queens imeshawapa taarifa wachezaji ambao haitakuwa nao msimu ujao na kati yao watatu wanahusishwa kujiunga na Yanga Princess.

Wachezaji hao ni kiungo Ritticia Nabbosa, Asha Djafar na Precious Christopher ambao mikataba yao kikosini hapo imeisha.

Asha Djafar aliyedumu kikosini hapo kwa misimu mitano mfululizo akiisaidia Simba kubeba mataji mbalimbali, amepewa taarifa hatakuwa sehemu ya kikosi msimu ujao kutokana na kupungua kwa kiwango chake msimu huu.

Kwa Nabbosa ambaye aliitumikia Simba kwa misimu miwili mfululizo, amekataa kuongeza mkataba mwingine licha ya viongozi kumuwekea ofa nzuri.

Nyota mwingine ni Precious ambaye ulikuwa msimu wake wa kwanza Msimbazi akitokea Yanga. Pia hadi sasa amekataa kusaini mkataba mpya.

Sasa inaelezwa wakati matukio hayo yakiendelea, Yanga imepeleka ofa ya maana kwa nyota hao watatu wakiwataka wajiunge na Wananchi.

“Kocha anawahitaji na tukiwasajili nyota hao wa kigeni itaongeza kitu kwenye kikosi chetu kutokana na uzoefu mkubwa walionao kwenye ligi,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:

“Tulipowafuatilia walituambia wamemaliza mikataba, ina maana wako huru kuzungumza na timu yoyote. Tunajaribu kuboresha baadhi ya maeneo kuelekea msimu mpya wa mashindano.”

Akiwa na Simba, Asha Djafar msimu wa 2021/22 aliibuka kinara wa ufungaji akiweka kambani mabao 27.

Related Posts