Dar es Salaam. Rishi Sunak, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, amerejea kwenye benki aliyokuwa akifanya kazi kabla ya kuingia kwenye siasa, atafanya kazi kama mshauri kwa takriban saa mbili kwa siku katika Benki ya Goldman Sachs.
Benki hiyo ya uwekezaji imetangaza kuwa Sunak, aliyeongoza Uingereza kuanzia Oktoba 2022 hadi Julai 2024, atawapa wateja wa kimataifa maarifa kuhusu masuala ya kiuchumi na kisiasa ya kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa, Sunak atafanya kazi kwa saa 70 kwa mwezi, ambazo ni sawa na takriban saa mbili kwa siku.
Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Goldman Sachs, David Solomon, ameelezea furaha yake kwa Sunak kurejea kwenye benki hiyo, akisema ana furaha kumkaribisha tena katika kampuni hiyo.
“Mbali na kuwashauri wateja, pia Sunak atakuwa akitumia muda na wafanyakazi wetu duniani kote, akichangia katika utamaduni wetu wa kujifunza na kujiendeleza kila mara,” amesema Solomon.
Mshahara wa Sunak utatolewa kama mchango kwa shirika la hisani la The Richmond Project, alilolianzisha mapema mwaka huu pamoja na mkewe, Akshata Murty, linalolenga kuboresha ujuzi wa hesabu kote nchini Uingereza.
Hata hivyo, ajira hiyo mpya ya Sunak imeelezwa kuwa na masharti kwa kuwa amewahi kushika nyadhifa nyeti ndani ya Serikali ya Uingereza.
Kamati ya Ushauri juu ya Uteuzi wa Kibiashara (Acoba), inayohusika na kuidhinisha kazi zozote zinazochukuliwa na mawaziri wa zamani kwa kipindi cha miaka miwili baada ya kuondoka madarakani, imeweka masharti na tahadhari maalumu kuhusu nafasi mpya ya Sunak.
Kamati hiyo imebainisha kuwa nafasi hiyo ina hatari kadhaa, ikiwemo uwezekano wa kuipa Goldman Sachs upendeleo usio wa haki wa kupata taarifa za ndani kutokana na uzoefu na nafasi aliyokuwa nayo Sunak wakati akiwa Waziri Mkuu.
Acoba imesema hali hiyo inaweza kuleta changamoto za kimaadili na kiusalama kwa mashirika ya kifedha.
Kwa mujibu wa Acoba, Sunak hataruhusiwa kushauri Serikali nyingine au mifuko yao ya uwekezaji ya kitaifa kwa niaba ya benki hiyo, wala kuwashauri wateja aliowahi kushughulika nao moja kwa moja alipokuwa Waziri Mkuu.
Pia, hataruhusiwa kushawishi Serikali ya Uingereza kwa niaba ya benki hiyo.
Acoba imebainisha kuwa Sunak aliwahi kufanya kazi katika sekta ya huduma za kifedha kwa miaka 14 kabla ya kuwa mbunge, ikiwa ni pamoja na kazi yake katika Goldman Sachs.
Sunak alizaliwa Mei 12, 1980 na wazazi wenye asili ya India waliozaliwa Afrika Mashariki. Baba yake alizaliwa katika Koloni la Kenya mwaka 1949, huku mama yake akizaliwa katika eneo la Tanganyika (ambalo sasa ni Tanzania).
Aliingia kwa mara ya kwanza katika benki hiyo kama mwanafunzi wa mafunzo (intern) mwaka 2000, kabla ya kuwa mchambuzi (analyst) kati ya mwaka 2001 hadi 2004.
Baadaye alishirikiana kuanzisha kampuni ya kimataifa ya uwekezaji.
Alichaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya kwanza mwaka 2015, na baadaye akahudumu kama Kansela wa Fedha wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Boris Johnson, wakati wa janga la Uviko-19.
Sunak alijizolea umaarufu alipokuwa akitangaza mipango yake katika mikutano ya waandishi wa habari wakati wa janga la Uviko-19.
Kujiuzulu kwake kama Kansela Julai 2022 kulichochea anguko la Serikali ya Waziri Mkuu, Boris Johnson.
Baada ya kipindi kifupi cha uongozi wa Liz Truss katika wadhifa wa Waziri Mkuu, Sunak alichukua nafasi hiyo Oktoba 2022.
Alihudumu hadi Julai 2024, wakati ambapo aliweka historia ya chama cha Conservative kushindwa kwa kishindo zaidi katika uchaguzi.
Kazi yake katika benki ya Goldman Sachs ni miongoni mwa majukumu mapya aliyoyachukua tangu aachie wadhifa wa Waziri Mkuu.