Tandahimba. Chama cha ACT-Wazalendo, kimedai kina majawabu ya changamoto zinazowakumba wakulima wa zao korosho nchini, ikiwemo bei ndogo na makato wanayokatwa wakati wa kuziuza.
Kimejinasibu kuwa majibu ya changamoto ikiwemo upatikanaji wa mbolea na soko la uhakika la zao hilo, yanayotokana na ACT Wazalendo kuwa na sera na muundo mzuri wa kuwatumikia wakulima.
Hayo yalielezwa kwa nyakati tofauti jana Ijumaa Julai 11, 2025 na viongozi wa ACT Wazalendo waliokuwa wakihutubia wananchi wa Tandahimba katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Shule ya Msingi, Matogolo mkoani Mtwara.
Viongozi hao wapo wakiongozwa na Zitto Kabwe na Ester Thomas (naibu katibu mkuu wa ACT Wazalendo Bara) wapo katika ziara ya siku 15 ya operesheni ya Majimaji Oktoba, Linda Kura iliyoanzia mkoa wa Tabora.
“Ukisikia matangazo ya mnada wa korosho, bidhaa hiyo inauzwa hadi Sh4,000, lakini ukitizama makato wanayokatwa kiuhalisia mkulima anabaki na Sh800 na yule anajitahidi anabakia na Sh1,200,”

“Leo hii mkulima wa korosho anatozwa fedha za magunia kati ya Sh110 hadi Sh120, pia anatozwa fedha ya usafirishaji wa korosho. Hivi vyote tutaviondoa ndio maana tunasema tuna majawabu ya changamoto hizi,” amesema Zitto.
Zitto amedai kuwa tozo na ushuru wanaolipa wakulima wa korosho upo juu hali inayosababisha kushindwa kumudu gharama za uendeshaji, jambo linalotafsiriwa ni ukandamizaji.
“Nimekuwa nikizungumzia ajenda hii kuanzia nikiwa bungeni hadi sasa bado sijachoka, ili mpate haki yenu rasmi,” amesema Zitto.
Kwa mujibu wa Zitto, chama hicho kimepiga mahesabu na kubainia asilimia 34 ya bei ya korosho ni tozo na ushuru, lakini wilaya zinazozalisha zao hilo bado hazijanufaika na uboreshaji na miundombinu.
“Newala na Tandahimba mnaongoza kwa kilimo cha korosho, mwaka jana zao hili limeingiza matrilioni kwa maana hiyo wakulima wa zao hili mnaingiza mabilioni ya fedha,” amesema Zitto.
Hata hivyo, Zitto amesema pamoja na wakulima kuingiza fedha zinazotokana na korosho, bado wananchi wao wanakabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo barabara ya kiwango cha lami inayodaiwa kujengwa kwa kususua.
Kabla ya Zitto kueleza hayo, mkazi wa Tandahimba, Juma Said ameiambia Mwananchi suala la miundombinu limekuwa kero katika jimbo hilo ili kuunganisha na wilaya ya Newala, akisema imekuwa ikijengwa kwa mafungu.
“Wakati Magufuli (hayati – Rais John Magufuli) ilianza kujengwa ikasimama, sasa hivi wakandarasi wapo kazini wanaendelea na majukumu ya ujenzi lakini wanasuasua na sisi tunapata shida ya vumbi,” amesema Shukuru.
Mei mwaka huu, Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega alikagua ujenzi wa barabara hiyo ya Mviwata – Newala hadi Masasi yenye kilomita 160 akisema imetengewa Sh230 bilioni ili kuzifungua wilaya za Tandahimba, Newala na Masasi.
Katika hotuba yake Zitto, amesema kwa muda wakulima wa korosho zao lenu limekuwa likiipatia fedha nyingi Serikali lakini hivi sasa ndio wakandarasi wanaonekana wakitekeleza ujenzi wa barabara hiyo.
“Licha ya hayo yote angalieni maendeleo ya mkoa wenu, wilaya zake hazijaunganishwa na lami, angalieni maendeleo ya miundombinu yenu, angalieni hali ya umasikini wa mkoa wenu halafu tofautisheni na mikoa mingine,” amesema Zitto.
Kutokana na hilo, Zitto amewataka wananchi wa Kusini kubadilika na kukichagua chama cha ACT Wazalendo ili kiwape majawapo wa changamoto zinazowakabili ikiwamo kuondoa na kufuta tozo na makato kwa wakulima.
Awali mjumbe wa Kamati Kuu wa ACT Wazalendo, Halima Nabalang’anya ameungana na Zitto akisema licha ya mkoa wa Mtwara kuwa na uzalishaji wa korosho, bado wananchi wanakabiliana na umasikini.
Mbali na hilo, wananchi wanakabiliana changamoto mbalimbali ikiwemo ubovu wa miundombinu hasa barabara zinazounganisha na wilaya za Tandahimba, Masasi hadi Newala ambako kunalimwa korosho kwa wingi.
“Sera ya ACT Wazalendo ni kupambania masilahi ya wananchi, kazi ambayo tutaifanya kwa sababu wao wameishindwa, tunataka Watanzania wakiwemo wa Tandahimba wapate huduma jamii,” amesema Nabalang’anya.